Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS KUJENGA MAJENGO YA KISASA VIWANJA VYA NDEGE VYA IRINGA, MANYARA NA TANGA


Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inajenga majengo ya kisasa ya abiria kwenye viwanja vya ndege vya Iringa, Lake Manyara na Tanga, imeelezwa.

Wahandisi wataalamu wa ujenzi wa viwanja vya ndege kutoka TANROADS wamewasilisha wasilisho la marejeo ya usanifu kwa Mfadhili wa miradi hiyo Benki ya Dunia, chini ya mpango wa Tanzania Transport Integration Project (TanTip), yenye lengo la kuboresha mtandao wa usafiri na usafirishaji nchini kwa kuunganisha maeneo ya utalii, uzalishaji na masoko kupitia miundombinu ya kisasa. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Wahandisi kutoka Mamlaka ya Usalama wa Anga (TCAA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

Wasilisho hilo linaonyesha kuwa majengo ya viwanja hivyo yatakuwa makubwa na ya kisasa kuliko yaliyopo na yatawezesha viwanja hivyo kuhudumia abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja tofauti na awali.

Majengo haya yatakuwa na maeneo ya biashara ikiwa ni pamoja na migahawa, maduka ya bidhaa mbalimbali, ofisi za mashirika ya ndege pamoja na ofisi za wafanyakazi wa viwanja hivyo.  Aidha, mnara wa kuongozea ndege.

Viwanja hivi ni miongoni mwa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambapo mbali na majengo kwa viwanja vyote vitatu pia kutajengwa barabara za kuruka na kutua ndege, majengo saidizi, mifumo ya kuongozea ndege kwa Viwanja vya ndege vya Tanga na Lake Manyara.

Kukamilika kwa viwanja hivi kutachochea kasi ya utalii ambapo kwa mikoa hiyo imekuwa na mbuga za wanyama za Ruaha, Manyara, Tarangire pamoja na mapango ya Amboni. 

TANROADS kupitia serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wa maendeleo kama Benki ya Dunia na makampuni ya kitaalam kuhakikisha miradi yote chini ya mpango wa TanTip inatekelezwa kwa ufanisi, na kukamilika kwa wakati, na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania kwa ujumla.