Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAWATOA HOFU WAFANYABISHARA


 

Serikali imewahakikishia wafanyabiashara wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa itaendelea kuboresha miundombinu na mifumo ya usafirishaji ili kurahisisha shughuli za usafiri na usarishaji wa abiria na mizigo baina ya mikoa hiyo na nchi jirani.

Akizungumza jjini Tanga mara baada ya ukaguzi wa maboresho ya reli inayoingia bandari ya Tanga Mkurugenzi wa Huduma za Huduma za Uchukuzi-Sekta ya Uchukuzi ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho ya Bandari ya Tanga, Mhandisi Aron Kisaka, amesema kukamilika kwa ukarabati na kukabidhiwa kwa sehemu ya gati lenye mita 300 lazima uende sambamba na maboresho ya miundombinu mingine ili kurahisisha utoaji wa mizigo bandarini.

“Kama wataalam tunazingatia sana utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yote hatuwezi kuboresha bandari hii tukaacha kutizama miundombinu saidizi iko kwenye hali gani, kwa hatua hii iliyofikiwa matokeo yameanza kuonekana ambapo ongezeko la mizigo kwa mwezi Septemba kwenda Oktoba limefika asilimia 41%,” alisisitiza Mha. Kisaka

Mhandisi Kisaka amesema lengo la Bandari ni kuhakikisha mzigo unaingia na kutoka kwa haraka ili kuongeza ufanisi na kuongeza zaidi shehena ya mzigo unaohudumiwa na bandari hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga, Mhandisi Masoud Mrisha, amesema utekelezaji wa mradi wa maboresho ya bandari hususani gati mbili unasimamiwa kwa karibu na unatarajiwa kukamilika mwezi aprili mwakani.

Mha. Mrisha ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi pamoja na miundombinu mingine bandarini hapo kutawezesha zaidi ya tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka na kutasababisha kushuka kwa bei za bidhaa mbalimbali sokoni.

Naye Mhandisi Patience Karumuna (wa kwanza kulia) kutoka Shirika la Reli Nchini (TRC) amesema kazi ya ukarabati wa reli kutoka stesheni ya Tanga mpaka bandarini ilikuwa umeshakamilka na kichwa cha treni kufanya majaribio lengo likiwa kubaini mapungufu yaliyobaki baada ya ukarabati.