Habari
SERIKALI YATOA AJIRA 1,000 BARABARA YA ‘RING ROAD’ DODOMA

Zaidi ya ajira 1,000 zimetolewa kwa wakazi wa jiji la Dodoma kupitia mradi wa kimkakati wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma (km 112.3) unaoendelea kutekelezwa Mkoani Dodoma.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi, Zuhura Amani katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo, ambao utekelezaji wake mpaka sasa umefikia asilimia 91.
“Katika utekelezaji wa mradi huu kumekuwepo fursa mbalimbali ikiwemo ajira zaidi ya 1,000 zimetolewa na zinaendelea kutolewa kulingana na kazi mbalimbali zinazoendelea, pia kampuni za ndani zinasambaza vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na mafuta”, ameeleza Mhandisi Zuhura.
Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba, 2025 kwa mujibu wa mkataba na unagharimu Shilingi Bilioni 221.7.
Aidha, Mhandisi Zuhura amebainisha ujenzi huo unahusisha barabara za njia nne za kiwango cha lami, madaraja makubwa, makalvati, njia za watembea kwa miguu pamoja na taa za barabarani kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Sambamba na mradi huo, Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa TANROADS inatekeleza miradi ambatishi ikiwemo upandaji wa miti zaidi ya laki moja na nusu (150,000) pembezoni mwa barabara hiyo ili kuhifadhi mazingira, ujenzi wa Shule ya Chilonwa (Ihumwa), vituo vinne vya afya na uchimbaji wa visima vinne vya maji.
Utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje inagusa maeneo ya Nala, Veyula, Mtumba na Matumbulu kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma na kuwa chachu ya ukuaji wa Makao Makuu ya nchi katika biashara, uwekezaji na utalii.