Habari
SERIKALI YATILIA MKAZO UWEKEZAJI WA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA VYUO VYA MAFUNDI SANIFU
Serikali imetilia mkazo uwekezaji katika teknolojia ya kisasa kwenye vyuo vya mafundi sanifu nchini ili kuongeza ujuzi, ubunifu na uwezo wa wataalamu hao kukidhi mahitaji ya soko la ajira linaloendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Hayo yamesemwa leo Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aisha Amour, wakati wa kufunga Mkutano wa Mwaka wa Mafundi Sanifu 2026 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Besta amesema mafundi sanifu ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan katika sekta ya ujenzi, miundombinu na viwanda, hivyo wanapaswa kuendelea kujifunza na kuendana na teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi na ubora wa kazi.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu na wadau wa sekta ya ujenzi kuhakikisha vyuo vya mafundi sanifu vinapata vifaa vya kisasa vya kufundishia pamoja na mazingira bora ya kujifunzia kwa vitendo.
“Teknolojia inaendelea kubadilika kwa kasi duniani, hivyo ni muhimu kwa mafundi sanifu kuongeza maarifa na ujuzi wa matumizi ya mifumo ya kisasa ili waweze kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi,” amesema Mhandisi Besta.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Bakari Mwinyiwiwa, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha mfumo wa mafunzo kwa vitendo kwa mafundi sanifu kwani hatua hiyo itasaidia kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.
Profesa Mwinyiwiwa amesema ERB itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi za elimu kuhakikisha mitaala ya mafunzo inaendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya sekta ya ujenzi na uhandisi.
Mkutano huo wa mwaka umezikutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya uhandisi, wakufunzi, wanafunzi pamoja na mafundi sanifu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili maendeleo ya taaluma hiyo na namna ya kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya taifa.
