Habari
SERIKALI YATANGAZA FURSA KWA VIJANA KATIKA SEKTA YA UJENZI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) pamoja na Bodi ya Usajili wa Wakadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo (AQRB) kuandaa mpango mahsusi wa kuwajengea uwezo vijana kwa nyenzo na ujuzi ili waanzishe Makampuni ya Ujenzi na Ushauri Elekezi zitakazoshiriki katika ujenzi wa miundombinu.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake inaandaa mpango wa kuwawezesha vijana kwa kuwajengea kesho iliyo bora “Building a Better Tomorrow (BBT)” katika kada ya Uhandisi, Ukandarasi, Wakadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo kwa kutenga miradi ambayo itawaongezea uzoefu katika kazi zao.
Bashungwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma Mei 23, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu Tanzania wa Mwaka 2024 ambao umeongozwa na Kauli mbiu “Matumizi ya Akili Mnemba kuongeza ufanisi: Kuimarisha Mafundi Sanifu kwa Changamoto zinazoibuka”.
“Wizara ya Ujenzi, tumepanga kuandaa mpango unaofanana na BBT kiuhandisi katika Sekta ya Ujenzi ili tuwawezeshe vijana wanaoungana katika makundi na kuanzisha Kampuni ambapo tutawapatia miradi ya kutekeleza na tutawasimamia kwa kuzingatia taaluma zenu kwa kuwalea hadi kuwa Kampuni kubwa”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amewaagiza mafundi sanifu wote nchini kuendelea kujisajili katika Bodi ya ERB kama yalivyo matakwa ya Sheria ili waweze kutambulika na kuwapo mazingira wezeshi katika fursa mbalimbali za miradi ya ujenzi inayoendelea hapa nchini ambapo amesisitiza kuwa idadi ya mafundi sanifu 2,785 iliyopo hivi sasa ni ndogo ikilinganishwa na wanaohitimu kila mwaka.
Kadhalika, Bashungwa ametoa rai kwa mafundi sanifu kuhakikisha ujuzi walionao usiishie kwenye Karakana zao kwa ajili ya maonesho bali warasimishe na kuingiza sokoni ili uweze kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii na kusaidia kupata kipato, kuendeleza vipaji vyao na kuanzisha kampuni zitakazochangia uchumi wa Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa uadilifu, kufanya kazi kwa mujibu wa maadili na miiko ya taaluma ya Kihandisi na kuwa tayari kuripoti wahandisi ambao wanakiuka maadili ili kuweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Naye, Msajili wa Bodi ya ERB, Mhandisi Bernard Kavishe, ameeleza dhumuni la mkutano huo ni kuwakutanisha mafundi sanifu kujadili mambo mbalimbali yanayohusu kada yao katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali iliyopo.
Kavishe ameeleza kuwa Bodi ya ERB imeandaa miradi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wanaomaliza vyuo vikuu kwenye kujifunza na miradi hiyo inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Septemba, 2024.
Mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu umehudhuriwa na Mafundi Sanifu takribani 800 na wengine 50 wakifuatalia mkutano huo kwa njia ya mtandao kutoka sehemu mbalimbali nchini huku Wahandisi 48 wamekuala kiapo cha Utii.