Habari
SERIKALI YAJIPANGA KUIMARISHA USAFIRI MAJINI

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inafanya mapinduzi makubwa katika kuboresha usafiri wa majini kwa kujenga meli na kusomesha wataalam anuai wa fani ya bahari.
Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya kozi ya ubaharia ambayo yamefadhiliwa na Taasisi ya Ushoroba wa Kati (CCTTFA) jijini Dar es Salaam amewataka wahitimu wa kozi hiyo, kuwa na nidhamu ili ujuzi walioupata uwe na manufaa kwa taifa na nchi za ushoroba wa kati kwa ujumla.
“Baharia mzuri ni yule mwenye nidhamu anapokuwa akitekeleza majukumu yake, maono na anayezingatia usalama wake, chombo na mali kwa ujumla,” amesisitiza.
Aidha amekitaka Chuo cha Bahari (DMI) kuhakikisha kinakuza mtandao wake na taasisi mbalimbali duniani ili kuwawezesha wanafunzi wa chuo hicho kupata muda wa kutosha wa kufanya mazoezi ya vitendo melini (Sea time).
Hata hivyo, Prof. Makame ameupongeza wakala wa ushoroba wa kati kwa kuwafadhili wanafunzi hao na kuahidi kutilia mkazo wa kuwa na mpango unaotekelezeka wa mafunzo kwa vitendo.
“Serikali tunajukumu kubwa la kuhakikisha wanafunzi wetu wa fani za bahari wanapata mafunzo kwa vitendo ya kutosha (Sea time) ili kuwaongezea ujuzi, kwenye utekelezaji wa kazi zao,”
Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane ameipongeza Tanzania kwa kutumia rasilimali zake katika kuhakikisha wahitimu wa nchi zote za ushoroba wa kati wanasoma na kuhitimu salama, na kusisitiza wahitimu hao kuwa wazalendo na kufikia malengo ya kuhimarisha huduma za usafiri majini.
Amezungumzia umuhimu wa nchi Wanachama wa Ukanda wa ushoroba wa Kati kutekeleza program walizojiwekea za kuimarisha usafiri na usafishaji hususani katika bahari na maziwa ili kukuza uchumi wa nchi zoo.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari DMI, Dk. Tumaini Gurumo amesema wahitimu hao wamepata mafunzo stahiki ambayo yatawawezesha kufanya kazi katika nchi zote zenye bahari na maziwa duniani.
Pamoja na hayo amezungumzia umuhimu wa kuwa na meli zinazomilikiwa na nchi wanachama wa ukanda wa ushoroba wa kati ili kuimarisha mazoezi ya vitendo kwa mabaharia.
Jumla ya wanafunzi kumi kutoka nchi wanachama wa Ushoroba wa Kati, ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda , DRC Kongonna Tanzania.