Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAELEKEZA BILIONI 60.1 KUJENGA BARABARA YA IRINGA - KILOLO


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa(Mb) amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa-Kilolo (km 33.61) kwa kiwango cha lami utakapokamilika utaleta mageuzi chanya na  kuchochea fursa nyingi katika Sekta ya Kilimo, Utali, Biashara na Uwekezaji.
 

Bashungwa ameeleza  hayo Oktoba 5, 2023 wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS), na Meneja Mkazi kutoka  kampuni ya Hunan Construction Engineering Group na kumtambulisha mkandarasi huyo kwa wananchi.

"Hakika historia inaenda kuandikwa kwani barabara ya Iringa - Kilolo imekuwa ni kilio cha muda mrefu, kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Iringa na hasa wale ambao walikuwa wawakilishi wenu kupitia Jimbo hili kwa nyakati tofauti tofauti pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wameisemea sana barabara hii", amesema Bashungwa.
 

Bashungwa ameongeza kuwa kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutawezesha wananchi kiuchumi, na kuwaondolea adha ya muda mrefu ya usafiri.
 

Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifahamu adha ya wana Iringa na mikoa jirani katika eneo la Kitonga na amemuagiza kufika na timu ya Watalaam kutoka TANROADS na kufanya tathimini ya ujenzi wa barabara ya mbadala ya muda mfupi wakati Serikali ikiendelea kutafuta dawa ya kudumu katika eneo hilo lenye mlima mkali.

Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass) yenye urefu wa kilometa 7.3 ambapo sasa hivi ipo katika hatua za manunuzi.


Bashunga amezitaja barabara zingine ambazo zitakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami katika mkoa huo ikiwemo barabara ya Iringa - Ipagala (km 71).
 

Aidha, Bashungwa ametoa agizo kwa TANROADS kuusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara hiyo ili ijengwe kwa viwango vilivyoanishwa kwenye mkataba ili tuweze kupata thamani ya fedha ambazo Serikali imewekeza na barabara hiyo idumu kwa muda uliokusudiwa.

Awali akitoa taarifa ya mradi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mha. Mohamed Besta amesema kuwa mradi huu utatekekelezwa kwa muda wa miezi 24 kwa gharama ya Bilioni 60.1


Ameeleza kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulianza mwezi Februari 2019 na kukamilika mwezi Julai, 2021 na kuanywa na Kampuni ya Inter-Consult ya Tanzania na umezingatia vigezo vyote vya kitaalamu.


Besta ameeleza kuwa mradi huu ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na Serikali  ikishirikiana na Benki ya Dunia katika mradi wa  Ushirikishaji na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) ikiwa ni mikakati ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Iringa.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa - Kilolo (km 33.61), ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Iringa kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta usafiri na usafirishaji