Habari
SERIKALI KUJENGA UPYA DARAJA LA MBWEMKURU NA NAKIU, LINDI
Serikali imesema inatarajia kujenga daraja lenye urefu wa mita 100 eneo la Mto Mbwemkuru lililopo mpakani mwa wilaya ya Ruangwa na Kilwa pamoja na daraja la Nakiu (mita 70), mkoani Lindi katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa mkoa huo.
Amesema hayo Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya Septemba 14, 2024 alipokagua miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo ambapo amesisitiza kuwa daraja la zamani ambalo limeharibiwa na mvua za El- Nino na Kimbunga Hidaya zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu litakarabatiwa na kutumika kwa muda wakati ujenzi wa daraja jipya ukiendelea.
“Tutajenga daraja lenye urefu wa mita 100 hapa kutoka na ukubwa wa mto huu, tupo katika hatua za manunuzi za kumpata Mkandarasi wa kujenga daraja hili, hivyo wananchi wa Lindi msiwe na wasiwasi kwani fedha zilishapatikana za kurudisha miundombinu hii”, amesema Kasekenya.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo unaenda sambamba na ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi Dar – es- Salaam pamoja na madaraja mengine yaliyoharibiwa na mvua hizo na Kimbunga Hidaya na kusisitiza kuwa hatua za kutafuta wakandarasi zinaendelea na ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa juhudi walizofanya ikiwemo kurejesha mawasiliano kwa madaraja na barabara zilizoathiriwa na mvua za El- Nino na Kimbunga Hidaya mkoani humo kwa muda mfupi.
“Nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya kurejesha miundombinu hii, Wizara imekuja kufanya tathmini kuona maeneo yaliyoathirika naamini utekelezaji utaanza mapema”, amesema Mkuu wa Mkoa.