Habari
SERIKALI KUBORESHA BARABARA NJOMBE
@Kero ya Usafiri Makambako–Songea Kumalizwa
Serikali imesema itaendelea kutekeleza na kuboresha miradi mbalimbali ya barabara mkoani Njombe ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa watu pamoja na mazao kufika sokoni kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.
Msigwa amesema Serikali inatambua kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Njombe wanategemea shughuli za kilimo kwa maisha yao ya kila siku, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, hususan katika maeneo ya vijijini yenye uzalishaji mkubwa wa mazao.
Amesema baadhi ya mashamba yako katika maeneo ya mbali yenye changamoto za usafiri, hali inayokwamisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni. Kutokana na hali hiyo, Serikali itaendelea kujenga na kuboresha barabara ili kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuongeza tija ya kiuchumi.
Aidha, Msigwa amesema Serikali inatambua kilio cha wananchi kuhusu hali ya barabara ya Makambako kwenda Songea ambayo imeharibika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri na wasafirishaji wa mizigo.
“Serikali imekamilisha taratibu zote muhimu, na muda si mrefu matengenezo ya barabara hiyo yataanza rasmi,” amesema Msigwa.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali pia imepanga kujenga maeneo maalum ya maegesho ya magari katika mji wa Makambako ili kuboresha huduma za usafirishaji na kupunguza msongamano wa magari.
Ameeleza kuwa kiasi cha shilingi milioni 108 kimetengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.
