Habari
RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI UKARABATI NA UPANUZI KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Rais Samia ameweka jiwe la Msingi leo Julai 16, 2024 ambapo ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ni mojawapo kati ya viwanja saba vinavyofadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na Wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa maendeleo ni hatua, hivyo Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Mkoa wa Rukwa ili kutatua changamoto za wananchi.
“Maendeleo ni hatua ikiwemo hatua hii kubwa ya ujenzi wa kiwanja cha ndege ndani ya Mkoa wa Rukwa, kila tunapoenda hatua moja ya maendeleo ndipo mahitaji mengine yanapotokea. Tutaenda hatua kwa hatua kuondosha changamoto za wananchi zinazojitokeza”, amesema Dkt. Samia.
Ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga utahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 30,000 kwa mwaka, ununuzi na usimikaji wa mitambo ya usalama na taa za kuongozea ndege, ujenzi wa mifumo ya kuondoa maji ya mvua kiwanjani, ujenzi wa barabara ya magari ya kuingia kiwanjani pamoja na maegesho ya magari.
Aidha, kazi nyingine itahusisha ujenzi wa uzio wa usalama kuzunguka Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga, ujenzi wa kituo kidogo cha umeme na ukarabati na upanuzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege kutoka kilometa 1.4 hadi kilometa 1.75, ujenzi wa kituo cha kufua umeme na ujenzi wa barabara ya kiungio (Taxiway) pamoja na maegesho ya ndege (Apron).
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa timu ya wataalam ya Wakala ya Barabara (TANROADS) imejipanga usiku na mchana kumsimamia Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group kuhakikisha wanafidia asilimia tano ya kazi zilizochelewa na kumuahidi Rais Dkt. Samia kuukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Machi, 2025.
Bashungwa amemueleza Rais Dkt. Samia kuwa ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege saba ukikamilika vitapelekwa Wizara ya Uchukuzi chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa ajili ya uendeshaji.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa utekelezaji wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ulianza tarehe 11 Septemba 2023 ambapo hivi sasa kazi zimefikia asilimia 17.14 ya utekelezaji.
Ameongeza kukamilika kwa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga utaruhusu ndege za abiria kati ya 50 na 60 kutua na kuruka kwa urahisi katika Kiwanja hicho.