Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

RAIS SAMIA AAGIZA BARABARA ZA MWANZA MJINI - USAGARA NA MWANZA MJINI - IGOMA KUFANYIWA USANIFU ILI KUJENGWA NJIA NNE.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Ujenzi kufanya Usanifu wa kina wa barabara za Mwanza Mjini hadi Round about ya Usagara na barabara ya Mwanza Mjini hadi Igoma ili zipewe kipaumbele katika bajeti ya Mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne.

Ameyasema hayo mkoani Mwanza leo tarehe 12 Novemba, 2023, wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ambapo ametembelea ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo- Busisi) ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 80.

“Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amenielekeza kufanya haraka sana usanifu wa kina wa barabara mbili, barabara ya Mwanza Mjini Kwenda Usagara Kilometa 22 na Mwanza Mjini kuelekea Igoma ili ziwekwe kwenye vipaumbele vya bajeti ya 2024/25 kujengwa kwa Njia nne”

Aidha, Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais tayari ametoa kibali  kwa mwaka huu wa fedha kujenga barabara ya kutoka Airport- Igombe hadi Nyanguge yenye urefu wa kilomita 46 iliyopo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 kwa kuanza kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 10.

Bashungwa ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa Daraja la JP Magufuli katika kuunganisha ushoroba wa Ziwa Viktoria unaoanzia Sirari mpakani mwa nchi ya Tanzania na Kenya hadi Mutukula Mpakani mwa Tanzania na Uganda, barabara hiyo itapanuliwa na kuwa na njia nne ili kupunguza msongamano wa magari.

“Mwelekeo huu  ni sambamba na kukamilika kwa daraja la JPM, Ujenzi wa SGR, Vivuko vinne vipya na vitano vinavyokarabatiwa, haya yote  yanaenda kulifanya jiji la Mwanza kuwa moja ya majiji bora ukanda huu wa Afrika” amesisitiza Bashungwa

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Paul Makonda, amesema daraja la JP Magufuli ni la kimkakati kwani mkoa wa Mwanza ni katikati ya nchi za Afrika Mashariki, hivyo itakuwa ni njia  ya mkato wa kufikia nchi jirani.

“Wananchi kutoka DRC, Uganda, Rwanda, Burundi wote watatumia daraja hili kufikisha bidhaa kwenye nchi zao pia kupitia ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR daraja hili litatumika kupitisha malori yenye mizigo mikubwa kufika huko”, amesema Makonda.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala, amesema ujenzi wa daraja hilo una manufaa makubwa na likikamilika utaokoa muda wa wananchi kusubiri vivuko kwani sasa watatumia dakika tatu hadi nne kuvuka kwenda upande wa pili wa Busisi.

Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mwanza Eng. Pascal Ambrose, amesema daraja hilo likikamilika litakuwa daraja la kwanza kwa ukubwa katika nchi za Afrika Mashariki na kati ambapo pia ni daraja la Sita kwa urefu barani Afrika.

Mbunge wa Sengerema, Mhe. Hamisi Tabasamu, amesema sambamba na ujenzi wa daraja hilo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha ujenzi wa barabara ya Sengerema hadi Irunda pamoja na ujenzi wa kivuko kipya ambacho kitakwenda kutoa huduma kutoka Buyagu-Sengerema  hadi Mbarika wilayani Misungwi.