Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUMILIKI MELI


Nchi za Afrika zimetakiwa kuwekeza katika umilikiwa wa meli kubwa za kusafirisha mizigo kutoka nchi za Ulaya kuja Afrika kutokana na ukuaji wa Biashara za Usafiri wa Majini duniani.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uchukuzi, Bw. Gabriel Migire kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wa usafiri toka Taasisi ya kikanda inayohusu usafirishaji Majini (ISCOS).

“Usafiri kwa njia ya Maji ni mkubwa zaidi ya shehena ya Mizigo asilimia kumi duniani inasafirishwa kwa njia ya maji hivyo ni muhimu nchi za Afrika kumiliki meli ili tuweze kusafirisha mizigo”, alisema Migire.

Aidha, Migire ameongeza kwa kusema kuwa serikali na watu binafsi wakimiliki meli itasaidia sana wanafunzi wanaosomea ubaharia katika vyuo vyetu  watakuwa na  nafasi kubwa ya kupata mafunzo na uzoefu  katika meli hizo hivyo ni muhimu nchi zetu kuwa na meli kubwa.

Mwakilishi kutoka kampuni  inayotengeneza Meli hapa nchini Songoro Marine  Godwin Isdori amesema kuwa Biashara ya Usafiri  kwa njia ya Maji ni kubwa hivyo ni Muhimu kwa Afrika  kumiliki Meli kwani Biashara hiyo inatoa ajira kubwa kwa vijana.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa wamiliki wa Meli Afrika Bi. Funmi Folorunso  kutoka Nigeria amesema ni muhimu kwa Serikali na watu binafsi kumiliki meli kwani ni usafiri unaotegemewa sana na kutoa  wito kwa watu binafsi na Serikali za Afrika  kuhakikisha zinamiliki meli  ili waweze kusafirisha mizigo na kuweza kupata pesa za kigeni katika nchi za Afrika.

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya kikanda inayohusu usafirishaji Majini (ISCOS) Daniel Kiyange amesema kuwa ni muhimu kwa waafrika kuwa na meli kwani taasisi hiyo kwasasa inaangalia namna mzuri ya kushirikisha nchi wanachama kununua na kumiliki meli

Taasisi ya kikanda inayohusu Usafiri Majini (ISCOS) inajumuisha nchi za Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda na Zambia.