Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

NCC YAFUNDISHA MBINU ZA KUTATUA MIGOGORO NJE YA MAHAKAMA


Serikali kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), imeendelea kutoa mafunzo kwa wadau wake mbalimbali, kuhusu utatuzi wa migogoro nje ya mahakama.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika Dar es Salaam kuanzia Juni 26, mwaka huu na kutoa mwangaza kwa washiriki kutoka kada mbalimbali za Sekta ya Ujenzi na zingine, ikiwemo ya biashara na Sheria.

Watoa mada, Bw Elias Kissamo ambaye ni Wakili wa Kujitegemea na Mkadiriaji Majenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi, na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Fauz Twaib,  wamesema kwa nyakati tofauti kuwa mbinu hizo mbadala za utatuzi wa migogoro ni dawa moja wapo ya kupunguza mirundikano ya kesi mahakamani.

Kwa mujibu wa Bw. Kissamo, Serikali umeona haja ya kuwa na mifumo mingine nje ya mahakama ya kutatua migogoro inayohusu Sekta ya Ujenzi na zingine, hivyo kuzipa baadhi ya taasisi zake jukumu la kuratibu na kusimamia utatuzi wa migogoro hiyo nje ya mahakama.

"NCC nayo inatekeleza jukumu hilo kwa kuchagua wasuhishi wa migogoro katika Sekta ya Ujenzi, miongoni mwa wasuluhishi walio kwenye mpangilio unaotambulika (registered arbitrators).

... pamoja hilo, inaendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali walio kwenye Sekta ya Ujenzi na nje ya sekta hiyo, ili wazijue mbinu hizo mbadala za kutatua migogoro, na kutokimbilia mahakamani kwa masuala yanayoweza kutatuliwa nje ya mahakama," Bw. Kissamo anasema.

Kwa upande wake, Dk.Twaib anasema kuna faida nyingi za kusuluhisha migogoro nje ya mahakama, kwa wahusika wa pande zote mbili zinazohusika na mgogoro.

Anasema, ili kuzijua faida hizo ni lazima mhusika awe angalau  na elimu fulani  kuhusu masuala hayo.

Dk Twaib anasema, matumizi ya muda mwingi mahakamani na gharama za kesi, vinaweza kupungua, ikiwa migogoro itatatuliwa nje ya mahakama, huku wahusika wakibaki na uhusiano mwema, tofauti na inavyokuwa wakipelekana kortini.

Dk Twaib amewashauri wadau kutoka sekta zote, ikiwemo ya ujenzi, kushiriki mafunzo yanayotolewa na Baraza la Taifa la Ujenzi Kwa sababu yana manufaa kwao na taifa kwa ujumla.