Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MWAKIBETE AWATAKA NIT KUONGEZA KOZI USAFIRI WA ANGA


Serikali imekitaka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kuhakikisha kinakamilisha taratibu za kupata ithibati na kuanza kufundisha kozi ya usafiri wa anga ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na idadi kubwa ya wataalam wanaoendana na ukuaji wa teknolojia nchini.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo maalum kwa Baraza la 12 la Uongozi wa Chuo hicho yanayofanyika mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema kuanza kwa kozi hizo kutaenda sambamba na kasi ya Serikali inayofanya kwenye ununuzi wa ndege nchini.

“Serikali inaendelea kununua ndege na ikumbukwe kuwa ndege hizi ni mpya hivyo uwepo wa ndege hizi bila kuwa na wataalam wa kutosha na chuo hiki tunacho hatutakuwa tunatenda haki, hivyo mjitahidi mwaka huu kozi zianze”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameeleza umuhimu wa Baraza hilo kuhakikisha maslahi ya watumishi yanazingatiwa ili kutoa motisha kwa uzalishaji wa wataalam wenye weledi na sifa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ameuhakikishia uongozi wa NIT kuwa Serikali itaendelea kuboresha Chuo hicho kwa kukiwezesha kwenye miundombinu ili kiweze kuzalisha wataalam wa kutosha kwenye njia zote za usafirishaji ikiwemo maji, anga na nchi kavu.

Kwa upande wake Mkuu wa NIT, Prof. Zacharia Mganilwa amemhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa Chuo hicho kiko tayari kuzalisha wataalam hao kwani sasa hivi kinaendelea na tafiti mbalimbali za kuhakikisha kinazingatia ubora kwenye uzalishaji wa wataalam.

Prof. Mganilwa amesema tayari kozi maalum imeanza kwa kuzingatia miradi mikubwa inayoendelea nchini ikiwemo wataalam wa reli ya Kisasa ya SGR, wahandisi na wahudumu wa ndege katika ngazi zote.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Utawala Hamid Mbegu, amesema Wizara imeendelea kuhakikisha chuo kinapata Baraza kwa wakati ili kutoathiri utendaji wake kwani Baraza hilo lina maamuzi kwa maendeleo ya chuo.