Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MWAKIBETE ATAKA WAHANDISI SGR KUPIMA VIFAA VYA UJENZI KIKAMILIFU


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amewataka Wahandisi wa Shirika ya Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR vinapimwa ubora wake kikamilifu kabla ya kutumika ili kuifanya reli hiyo kudumu kwa mika mia moja (100).

Akizungumza jijini Mwanza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Sehemu ya Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa Kilomita 249 Naibu Waziri Mwakibete, amesema thamani ya mradi huo itapimwa kupitia reli hiyo kufikia muda uliokusudiwa.

“Kwa fedha tulizowekeza hapa zaidi ya takribani trilioni tatu (3) sitegemei kama wataalam tutakubali nondo, simenti na vifaa vingine vitumike ambavyo havina viwango na niwakumbushe tu reli hii ikidumu mtakumbukwa na Taifa hili” amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TRC kupitia kitengo cha Masoko kuanza kufanya tafiti za kina kwa mzigo utakaosafirishwa kupitia reli hiyo kwani mikoa kama shinyanga kuna migodi na nchi Jirani kama Uganda zina mzigo mkubwa ambao zinaweza kuitumia reli hiyo kupitia Mwanza.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ametoa rai kwa wananchi wanaoishi katika maeneo inapojengwa reli hiyo kujiepusha na vitendo vya wizi wa mafuta, simenti ili kutokwamisha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja Mradi Sehemu ya Isaka hadi (Mwanza KM 249) Eng. Machibya Shiwa, amemhakikishia Naibu Waziri kuwa changamoto za upimaji zitaimarishwa pamoja na usimamizi kwani TRC imeongeza watalaam wa kutosha ili kuhakikisha maeneo yote yanasimamiwa

Eng Machibya ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo mpaka mwezi oktoba 2022  umefikia asilimia 17 na kazi zinazoendelea kwa sasa ni kukamilisha kujenga tuta la reli ambayo ndio kazi kubwa kwenye ujenzi.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete yuko jijini Mwanza kwa ziara ya siku mbili (2) inayohusisha ukaguzi wa miradi na kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ili kuona utendaji kazi wake.