Habari
MKOA WA RUVUMA NA MKOA WA MOROGORO KUUNGANISHWA KWA BARABARA YA LAMI

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inatarajia kuanza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro kwa barabara ya lami.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa ambayo tayari wilaya zake zote zimeunganishwa kwa lami na makao makuu ya Mkoa.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi amesema serikali inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Lumecha – Londo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hadi Kilosa – Kidatu mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.
Mhandisi Mlavi ameutaja mradi huo kuwa utahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilometa 512 ambao ukikamilika utaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro kwa kiwango cha lami .
“Mradi huu upo katika hatua ya kupitia zabuni za wakandarasi ambapo zabuni hizo zilifunguliwa tarehe 26 Agosti 2022”, amesema Mhandisi Mlavi.
Ameongeza kuwa Mradi huo utatekelezwa kwa kutumia mtindo wa Usanifu, Manunuzi, Ujenzi na Ufadhili (Engineering,Procurement, Construction and Financing.
Hata Hivyo Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajia kuanza muda wowote baada ya hatua stahiki za manunuzi kukamilika.
Akizungumzia ujenzi wa Barabara ya Songea – Makambako kwa kiwango cha lami, Mhandisi Mlavi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatarajia pia kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya lami sehemu ya Songea – Lutukira ikijumuisha na sehemu ya Mtwara korido yenye urefu wa kilometa
111.
Mhandisi Mlavi amesema katika utekelezaji wa mradi huo,Serikali tayari imeshaingia makubaliano na Mfadhili ambaye ni Benki ya Dunia na hivi sasa utekelezaji wa mradi huo upo katika hatua za awali za manunuzi.
Amebainisha kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kilometa 111 za lami ambazo zitajumuisha kilometa 14 za Songea bypass katika Manispaa ya Songea na ujenzi wa barabara ya Songea hadi Lutukira Halmashauri ya Madaba yenye urefu wa kilometa 97 hivyo kuunganisha wilaya ya Songea mkoani Ruvuma na wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Hata hivyo amesema kuwa Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya ya Nyasa tayari umeunganishwa na Mkoa wa Njombe kupitia wilaya ya Ludewa kwa kutumia daraja la mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa.
Amesema mradi wa daraja la Ruhuhu ulianza kutekelezwa Juni 2016 na kukamilika Oktoba 2021 kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 8.9 ambao umeunganisha wilaya za Nyasa na Ludewa.