Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MKOA WA KIGOMA UTAKUWA MWANZO WA RELI KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Kigoma ili kuufanya Mkoa huo kuwa mwanzo wa reli na sio mwisho wa reli katika Sekta ya Miundombinu.

Bashungwa ameeleza hayo leo Julai 08, 2024 mbele ya wananchi wa eneo la Kazuramimba katika ziara ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ya ukaguzi wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Malagarasi - Ilunde - Uvinza Mkoani Kigoma.

“Ni maelekezo yako Mheshimiwa Makamu wa Rais, umechoka na ule usemi wa Kigoma mwisho wa reli, badala yake Kigoma iwe mwanzo wa reli na sisi Wizara ya Ujenzi tunaenda kutekeleza hilo kuhakikisha mkoa huu unakuwa Mwanzo wa reli katika sekta ya Miundombinu”, amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imekamilisha kufanya usanifu wa barabara kuanzia Kibaoni kuelekea Kasulu na hatua iliyopo hivi sasa ni kuendelea kufanya mazungumzo na mfadhili ili nayo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais nikuahidi Wizara ya Ujenzi hatutakuwa kikwazo kwa dhamira yako ya kusaidia Mkoa wa Kigoma kupata maendeleo, kwahiyo barabara hii ya kibaoni kwenda Kasulu tunaendelea na mazungumzo ili tutakapokamilisha ujenzi wa kilometa 51.1 ya barabara ya Malagarasi - Uvinza basi na kipande cha Kibaoni - Kasulu kianze kujengwa kwa kiwango cha lami”, amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa Mkoa wa Kigoma utaunganishwa na Mkoa wa Katavi kwa barabara ya lami hivyo wizara ya ujenzi itakamilisha usanifu wa kina wa kilometa 102 zilizobakia ili Serikali iweke katika vipaumbele vyake na kutengewa bajeti.