Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA CHACHU YA MAENDELEO SIMIYU


Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na unapakana na mikoa ya Mara, Mwanza, Singida na Shinyanga jina la Simiyu limetokana na Mto Simiyu, ambao ni miongoni mwa mito muhimu inayopita katika eneo hilo na kuelekea Ziwa Victoria.

Mkoa huo ulianzishwa kupitia mchakato wa kisheria wa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala na kupewa nguvu kisheria kupitia Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 72 la Machi 2, 2012, kabla  ya kuanzishwa kwake, eneo linalounda Mkoa wa Simiyu lilikuwa sehemu ya Mkoa wa Shinyanga na lilijumuisha wilaya tano za Bariadi, Maswa, Busega, Meatu na Itilima.

Kwa mujibu wa takwimu za mtandao wa barabara mkoani humo, Simiyu ina jumla ya kilomita 4,730.95 za barabara zinazohusisha barabara kuu, za mikoa, wilaya na vijijini kati ya hizo, barabara kuu zina urefu wa kilomita 334.72, barabara za Mikoa kilomita 532.30, barabara za Wilaya kilomita 2,420.50 na barabara za Vijijini kilomita 1,451.53.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Boniface Mkumbo, anasema uboreshaji wa miundombinu hiyo umeendelea kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na usafirishaji.

 

BARABARA ZAFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI

Uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Simiyu umeendelea kuwa chachu ya maendeleo, kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko na kuwawezesha wananchi kufikia huduma muhimu za kijamii na kiuchumi.

 

Kwa mujibu wa Mhandisi Mkumbo, mkoa huo una barabara kuu mbili zinazounganisha Simiyu na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kati ambapo barabara hizo ni Mwanza–Mara yenye urefu wa kilomita 58.6 inayopita katika Mkoa wa Simiyu na barabara ya Lamadi–Bariadi–Maswa hadi mpakani mwa Shinyanga yenye urefu wa kilomita 155.

Aidha, Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) umeendelea kutekeleza miradi ya kuboresha barabara za mikoa, ikiwemo kipande cha Maswa–Bariadi chenye urefu wa kilomita 49.7 kilichojengwa kwa kiwango cha lami.

Serikali pia inaendelea na maandalizi ya kutekeleza miradi mingine ya barabara, ikiwemo Barabara ya kutoka Bariadi–Salama–Gh’aya–Magu yenye urefu wa kilomita 76, Nyashimo–Ngasamo–Ndutwa kilomita 48 na Karatu–Mbutu–Hydom–Mto Sibiti–Meatu–Lalago–Maswa yenye urefu wa kilomita 339.

Miradi hiyo inalenga kuongeza muunganiko wa Simiyu na mikoa jirani, kurahisisha usafirishaji wa mazao na mifugo na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.

Mhandisi Mkumbo anasema mpango wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) ni kuhakikisha Mkoa wa Simiyu unafunguliwa zaidi kwa barabara za lami, huku Serikali ikiendelea kuunganisha mikoa kwa miundombinu hiyo katika hatua hiyo TANROADS imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mkoma–Lalago yenye urefu wa kilomita 65.

Aidha, barabara ya Bariadi–Itilima–Kisesa–Mwandoya hadi Ngoboko yenye urefu wa kilomita 102 ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, huku hatua za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo zikiendelea.

Mradi huo ukikamilika unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Bandari ya Tanga kwenda nchi jirani za Rwanda,Burundi na Congo pamoja na mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na maeneo ya Kaskazini, hivyo kuongeza fursa za shughuli za kiuchumi.

 

MADARAJA YAIMARISHA MAWASILIANO

Mbali na barabara, Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa madaraja, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya usafiri, hasa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yakikumbwa na changamoto wakati wa msimu wa mvua.

Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu imefanikiwa kujenga madaraja 28 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,miongoni  mwa madaraja hayo ni daraja la Itembe, Mwakisandu na Mwakagula, ambayo yameendelea kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa usafiri mkoani humo.

Daraja la Itembe lina urefu wa mita 150 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita moja, ujenzi wa daraja hilo umeimarisha mawasiliano na kurahisisha usafirishaji wa mazao na mifugo kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda katika masoko.

Aidha, Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 160 limejengwa katika barabara ya Bariadi–Mwangongo–Mwanhuzi–Sibiti hadi Singida, likiwa sehemu ya juhudi za kuimarisha muunganiko wa Simiyu na maeneo mengine ya nchi.

Kwa wananchi wanaotumia miundombinu hiyo, maboresho ya barabara na madaraja yamepunguza changamoto za usafiri zilizokuwa zikijitokeza wakati wa mvua, ambapo baadhi ya maeneo yalikuwa yakipitika kwa shida kutokana na kujaa kwa maji,hali hiyo imechangia kurahisisha shughuli za biashara, huku wafanyabiashara wakiweza kusafirisha bidhaa kati ya Simiyu na mikoa jirani kwa urahisi zaidi.

 

TANROADS YAIMARISHA USALAMA BARABARANI

Katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara, TANROADS Mkoa wa Simiyu imeendelea kuweka miundombinu mbalimbali, ikiwemo taa za barabarani na taa za kuongozea magari katika maeneo ya makutano, hasa katika Makao Makuu ya Mkoa, Bariadi.

 

Jumla ya taa 800 zimewekwa katika miji na vituo mbalimbali, ikiwemo Makao Makuu ya Mkoa mjini Bariadi na Wilaya ya Maswa.

Aidha, TANROADS imejenga maeneo mawili ya mapumziko kwa wasafiri na maeneo mawili ya maegesho ya magari katika Mji wa Bariadi, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya watumiaji wa barabara.

TANROADS YAJIANDAA KUKABILI ATHARI ZA MVUA

Kwa kuzingatia changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua za vuli pamoja na mvua zinazoweza kuambatana na hali ya El Nino TANROADS imeendelea kufanya ukaguzi wa barabara, madaraja, makalavati na maeneo mengine hatarishi mkoani humo.

Ukaguzi huo unalenga kutathmini utayari wa miundombinu kukabiliana na athari za mvua, kuchukua hatua za kinga na kuhakikisha maeneo yenye changamoto yanashughulikiwa mapema.

Hatua hiyo inalenga kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua na kuhakikisha miundombinu inaendelea kuwa salama na kupitika.

Kwa ujumla, uwekezaji katika barabara na madaraja mkoani Simiyu unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usafiri na usafirishaji, kukuza biashara na kuwaunganisha wananchi na masoko pamoja na huduma za kijamii.

Ni wazi kuwa, kadiri mtandao huo unavyoendelea kuboreshwa, miundombinu hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wananchi katika shughuli za uzalishaji, biashara, kilimo na ufugaji, huku ikiimarisha muunganiko wa Simiyu na mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kati.