Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

DKT.MWIGULU ATAKA KIVUKO CHA MV. KIKOVE KUFIKA MALINYI JANUARI 5


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya, kuhakikisha kivuko cha MV. Kikove kinafika Malinyi ifikapo Januari 5, 2027 na kuanza kutoa huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Malinyi na Mlimba.

Agizo hilo amelitoa leo, Naovemba 24, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Toboatobo, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, alipofika kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao na kuzitafutia ufumbuzi.

Dkt. Mwigulu amesema haikubaliki kivuko hicho kuchukua takribani miaka tisa kujengwa huku wananchi wakiendelea kukabiliwa na adha ya usafiri na kushindwa kufikia kwa urahisi huduma mbalimbali za kijamii.

“Mimi sitaki ngonjera, fedha ilishalipwa. Miaka tisa hatuwezi kuzungumzia jambo hili tena, Wananchi wamekaa muda mrefu kusubiri kivuko, wengine wanapoteza maisha kwa kuliwa na mamba kwa sababu ya kukosa kivuko,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu amesema amepokea ombi la wananchi hao la ujenzi wa barabara ya Ifakara–Malinyi na kuahidi kusimamia utekelezaji wake ili ijengwe na kukamilika kwa wakati.

“Hii ni barabara ya kiuchumi, kwa hiyo Serikali itaisimamia ili ijengwe. Tutaweka uzito ili mkandarasi alipwe malipo yake ya awali na aanze kazi,” amesema Dkt. Mwigulu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema amezungumza na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ambaye amemhakikishia kuwa kivuko cha MV. Kikove kimekamilika na kitafika Malinyi Januari 5, 2027 kikitokea Mwanza, kilikokuwa kikitengenezwa, tayari kwa kuanza kutoa huduma.

Kuhusu barabara ya Malinyi–Ifakara, Mhandisi Kasekenya amesema tayari imeingizwa kwenye mpango wa ujenzi, huku kinachosubiriwa kikiwa ni upatikanaji wa fedha za kuanza kazi, kwani mkandarasi tayari amesaini mkataba.

Naye, Mbunge wa Malinyi, Mecktridis Mdaku, amesema kilio kikubwa cha wananchi wa Malinyi ni kupatiwa kivuko cha MV. Kikove ambacho ujenzi wake umechukua muda mrefu kukamilika.

Aidha, ameiomba Serikali kuipa kipaumbele Malinyi kwa kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kijamii.