Habari
MAANDALIZI UJENZI WA BARABARA YA LONGIDO- SIHA KM 53 NA ELERAI-KAMWANGA KM 39.5 YAIVA
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemweleza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Longido- Siha km 53 na Elerai-Kamwanga km 39.5 yamekamilika kinachosubiriwa ni malipo ya awali ili ujenzi huo uanze.
Amemhakikishia kuwa barabara hizo licha ya kuunganisha wilaya za Longido (Arusha) na Siha (Kilimanjaro) pia ni njia fupi ya kuuzunguka mlima Kilimanjaro hivyo kukamilika kwake kwa lami kutachochea huduma za utalii katika ushoroba wa kaskazini yaani Serengeti, Ngorongoro na mlima Kilimanjaro.
"Tumekamilisha usanifu na ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa barabara hizo zijengwe ili kuimarisha kwa njia fupi ushoroba wa utalii", amesema Eng. Kasekenya.
Naibu Waziri Kasekenya alikuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Sinya wilayani Longido katika ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba inayoendelea Mkoani Arusha.
