Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA KUPANULIWA KUFIKIA MITA 3000


Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kwa kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kutoka ya sasa yenye mita 1800 hadi kufikia mita 3000 kutaruhusu kiwanja hicho kuhudumia ndege kubwa zaidi zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 150.

 

Akizungumza mkoani Kigoma mara baada ya kutembelea Kiwanja hicho Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali imedhamiria kufufua usafiri wa anga nchini kwa kununua ndege na kuboresha viwanja vya ndege ili kurahisisha shughuli za biashara na utalii baina na mikoa na nchi Jirani.

 

“Serikali inaendelea na mkakati wake wa kuendelea kujenga viwanja vya ndege nchini hasa ukizingatia Mhe Rais alifanya filamu ambayo matokeo yake yameanza kuonekana na hatuna budi kuendelea kujenga miundombinu rafiki na mizuri kwenye kila eneo’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

 

Naibu Waziri Mwakibete amewapongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa kuendelea kufanya maboresho katika viwanja mbalimbali nchini na kuwataka kuendelea kushirikiana na vyombo vingine ili kuhakikisha wanadhibiti usafirishaji wa nyara za Serikali.

 

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini Kilumbe  N’genda ameishukuru Serikali na kusema Kigoma itaendelea kufunguka kibiashara na kukuza pato kwani nchi Jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Burundi zinafanya sana biashara na mkoa wa Kigoma.

 

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma Mbura Daniel amesema idadi ya miruko ya ndege imekuwa ikiongezeka kwani hicho pamoja na kutumiwa na ndege za ratiba kama Air Tanzania pia mashirika mbalimbali hukitumia kiwanja hicho kwa kuja kufanya biashara na mikutano ya Kimataifa.

 

Meneja wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Mkoa wa Kigoma Mwantum Kipwasa amesema shirika linasubiri kwa hamu kukamilika kwa upanuzi huo ili kuleta ndege kubwa kwani idadi ya abiria imelazimisha shirika hilo kuwa na ndege kila siku ili kukidhi haja ya wateja wao.

 

Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege unatarajiwa kugharimu zaidi ya bilioni 50 na fedha hizo zitahusisha upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho, uzio na malipo ya fidia.