Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KILOMITA 603 ZA BARABARA ZAENDELEA KUJENGWA NCHINI


IMEELEZWA takriban miradi 16 ya ujenzi wa barabara yenye gharama ya shilingi trillion 1.4, sawa na kilomita 603 inaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kuimarika na kuleta tija kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema hayo leo wakati akikagua maendeleo mradi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka BRT III jijini Dar es Salaam.

Eng. Mativila ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Barabara ya Mianzini-Olemringaringa-Sambasha KM 18, Ntendo-Muze-Kilyamatundu KM 179, na Malagarasi-Ilunde-Uvinza KM 51.1.

Mingine ni Barabara ya Karatu-Mbulu-Hydom-Sibiti-Lalago-Maswa KM 389, Matai-Kasesya KM 50, Ntyuka-Mvuni KM 76 na barabara ya Tarime-Mugumu KM 87.14.

Eng. Mativila amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara za lami na madaraja ya kisasa katika kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote na hivyo kuleta tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ujumla.

"Nawahakikishia wakazi wa Dar es salaam Barabara ya BRT II, na BRT III zitakamilika kwa mujibu wa mpango tuliouweka ili kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katikati jijini la Dar es Salaam," amesisitiza Eng. Mativila.

Aidha amewataka mameneja wa TANROADS nchini kote kuhakikisha barabara zinapendezeshwa na kuwa katika hali bora wakati wote.

Kwa upande wake Meneja wa barabara za BRT Eng. Barakaeli Mmari amesema wamejipanga kuhakikisha magari yanaongozwa vizuri katika barabara zinazojengwa ili kupunguza msongamano wa magari na kuepuka ajali.