Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KATIBU MKUU UCHUKUZI ASISITIZA USIMAMIZI MIRADI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire amewataka wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Sekta hiyo kuhakikisha zinasimamia miradi mbalimbali ya maendeleo  inayotekelezwa chini ya taasisi zao zinakamilika kwa wakati na kwa viwango.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la utiaji saini mikataba ya utendaji kwa Mwaka 2023/24 baina yake na Wakuu wa taasisi, Migire amesema ufutailiaji na usimamizi utapunguza ucheleweshaji hasa kwenye kukamilika kwani changamoto zitakazobainika wakati wa utekelezaji zitapatiwa ufumbuzi mapema.

“Wataalam wapo kwenye kaguzi kila siku, lakini utashangaa viongozi wakuu wakikagua miradi ndio wanabaini changamoto zilizopo, nendeni mkawatumia wataalam hao vizuri na kuwepo na ratiba maalum zinazotambulika za ukaguzi ili mbaini changamoto mapema na kuzitafutia ufumbuzi mapema pia’ amesema Katibu Mkuu Migire.

Aidha,Katibu Mkuu Migire amesisitiza pia umuhimu wa nidhamu katika matumizi ya fedha ambapo amesema ni jukumu la wakuu wa taasisi kuhakikisha fedha zinatumika vizuri kwa kuweka vielelezo sahihi baada ya matumizi ili kupunguza hoja ambazo zimekuwa zikiibiwa kila mwaka na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ufatiliaji na Tathmini Sekta ya Uchukuzi, Bi Devota Gabriel amesema tathmini iliyofanyika kwa mwaka 2022/23 imeonyesha taasisi zimefanya vizuri kwenye usimamizi wa miradi na mafunzo kwa watumishi hali inayoongeza morali za watumishi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO) Bi. Christina Mwakatobe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka vigezo kwa wakuu wa taasisi kwani vinawafanya kujitathmini katika utendaji kwa kila hatua ya utendaji.

Zoezi la Utiaji saini kwenye utendaji limefanya kati ya Katibu Mkuu na Wakuu wa taasisi zaidi ya kumi na moja zinazosimamiwa na Sekta ya Uchukuzi.