Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AWATAKA WANANCHI KUHESHIMU ALAMA ZA BARABARANI KUPUNGUZA AJALI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya, amewataka wananchi na wasafirishaji kuzingatia na kutii alama za barabarani ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Ametoa wito huo leo, Novemba 27, 2026, wakati akifunga Kongamano la Afrika kuhusu Usalama Barabarani (Africa Road Safety Summit) lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili mikakati na mapendekezo ya kupunguza ajali za barabarani nchini.

“Tunahitaji kuondokana na janga la ajali za barabarani, iwe kwa waendesha bodaboda au madereva wa magari, kwa kuhakikisha kila mmoja anaheshimu alama za barabarani anazokutana nazo katika safari yake,” amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amesisitiza umuhimu wa jamii kuacha tabia ya kuondoa au kuharibu alama za barabarani, akieleza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kuchangia kutokea kwa ajali.

Amewapongeza  Taasisi ya Usalama Barabarani Tanzania (TARSI), ambao ni waandaaji wa kongamano hilo,  kwa kuandaa jukwaa hilo ambalo litasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usalama barabarani.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kisasa ya barabara inayozingatia uwekaji wa alama za barabarani pamoja na miundombinu maalumu kwa watembea kwa miguu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usalama na kupunguza ajali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usalama Barabarani Tanzania (TARSI), Maliki Barongo, amesema kuwa lengo la kuandaa kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri na miundombinu ili kujadili kwa pamoja mikakati na njia bora za kupunguza ajali za barabarani nchini.

Ameongeza kuwa TARSI itawasilisha Serikalini mapendekezo yaliyotolewa na wadau wakati wa kongamano hilo ili yaweze kufanyiwa kazi na kusaidia kuimarisha usalama barabarani.

Kongamano hilo limewashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawakilishi wa Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Jeshi la Polisi, ambao wamejadili na kutoa maoni kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto ya ajali za barabarani.