Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AWATAKA WAKANDARASI WANAWAKE KUUNGANA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itaendelea kutenga miradi ya ujenzi kwa ajili ya wakandarasi wanawake ili kuwawezesha wakandarasi hao kupata uzoefu, kukuza mitaji na kutoa fursa kwa Watanzania.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakandarasi Wanawake jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakandarasi wanawake wanaimarika na kutekeleza miradi mingi ya Serikali ambayo inatekelezwa nchini.

“Chapeni kazi, pia kamilisheni miradi kwa wakati ili Serikali iwaamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata kazi nyingi zitakazowainua kiuchumi kama walivyo makandarasi wengine”, amesema Eng. Kasekenya.

Aidha, amewataka wakandarasi wanawake kuwa waaminifu na waadilifu ili kuaminiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha na kuweza kupata mikopo kwa urahisi  hatimaye kukuza mitaji yao.

Amezungumzia umuhimu wa Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuwajengea uwezo wakandarasi wanawake ili wamudu kutekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi midogo na mikubwa.

“Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza miradi mingi ya miundombinu hivyo unganeni jengeni uhusiano mzuri na taasisi mbalimbali ili mpate kazi,” amesema Kasekenya.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake, Eng, Judith Odunga, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotoa vipaumbele vingi kwa wakandarasi wanawake na kusisitiza utaratibu huo ukiendelea uchumi kwa wakandarasi wanawake utakuwa na kuchochea maendeleo ya nchi.

Huu ni mkutano Mkuu wa Tatu kufanyika kwa wakandarasi wanawake, ambapo mkutano huu hufanyika mara moja kwa mwaka lengo likiwa ni kuwakutanisha pamoja, kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.