Habari
KASEKENYA AWAASA WAHANDISI KUWA WAADILIFU, KURITHISHA UJUZI KWA VIJANA
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wahandisi nchini kuwa wachapakazi, waadilifu na waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha kazi wanazozifanya zinakuwa na ufanisi, weledi na tija kwa taifa.
Kasekenya ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya 23 ya Siku ya Wahandisi Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City.
Amesema wahandisi ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kutumia taaluma, maarifa na ubunifu wao kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.
Mhandisi Kasekenya amesema Serikali inahitaji taaluma ya uhandisi yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, akibainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ikiwamo barabara, madaraja, reli, majengo na viwanja vya ndege unategemea kwa kiasi kikubwa utaalamu wa wahandisi.
“Tugeuze maarifa kuwa vitendo, tubadili changamoto kuwa fursa, tutumie teknolojia kuongeza tija na tutumie uhandisi kujenga Tanzania yenye nguvu, salama na endelevu,”amesema Kasekenya.
Aidha,amewataka wahandisi kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa katika kubuni na kujenga miundombinu, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa vitendo, tafiti na ubunifu ili kupata suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi.
Kasekenya pia aliwasisitiza wahandisi wenye uzoefu kuhakikisha wanawarithisha vijana maarifa na ujuzi walioupata katika taaluma hiyo, hatua ambayo amesema itasaidia kujenga kizazi kipya cha wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya maendeleo ya taifa.
Maadhimisho ya 23 ya Siku ya Wahandisi Tanzania yalianza Septemba 23, 2026 na kufikia kilele Septemba 25, 2026, yakiwa na shughuli mbalimbali, ikiwamo kutambua na kutoa vyeti kwa wadhamini walioshiriki kufanikisha maadhimisho hayo.
