Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA ATOA MIEZI 10 UJENZI MADARAJA YA CHAKWALE NA NGUYAMI MKOANI MOROGORO


Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ametoa miezi 10 kwa Mkandarasi M/s Asabhi anayejenga daraja la Chakwale mita 80 na M/s Koberg anaejenga daraja la Nguyami 100m kuhakikisha yanakamilika kwa ubora uliosanifiwa.

Madaraja hayo yako katika barabara ya Iyogwe- Chakwale-Ngilori (Gairo), yenye urefu wa km 41 ambayo inaunganisha mkoa wa Tanga- Morogoro-Dodoma kwa njia fupi.

" Fedha zipo hivyo hakikisheni madaraja haya yanakamilika kwa ubora uliokusudiwa ili yaweze kubeba magari makubwa na pindi barabara ya lami itakapojengwa yasifanyiwe marekebisho", amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amewataka wakazi wa wilaya za Gairo mkoani Morogoro na Kilindi mkoani Tanga kuzalisha mazao mengi ili uwekezaji unaoendelea uwanufaishe kiuchumi.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Morogoro Eng. John Mkumbo amesema watahakikisha madaraja hayo na barabara unganishi mita tano kila upande yanakamilika kwa wakati.

" Tutawasimamia wakandarasi hawa kikamilifu ili miradi hii  iwiane na thamani ya fedha na hivyo kuleta tija kwa wananchi",amesema Eng. Mkumbo.

Zaidi ya shilingi bilioni 6.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa daraja la Chakwale lenye urefu wa mita 800 wakati shilingi 7.1 Bilioni zikitarajiwa kutumika katika daraja la Nguyami lenye urefu wa mita 100.