Habari
KASEKENYA ATAKA UJENZI WA BARABARA YA ISONGOLE -ISOKO KM 52 UENDE KWA KASI

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameutaka wakala wa barabara nchini TANROADS mkoa wa Songwe kumsimamia kikamilifu Mkandarasi anaejenga barabara ya Isongole-Isoko km 52 ili ikamilike kwa wakati.
Kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Ileje na kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi.
Ameyasema hayo leo Wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana na wanawake wa eneo hilo la mradi.
"Msimamieni Mkandarasi vizuri, tunatamani anavyoanza kwa kasi asimamiwe kwa kasi hiyo hiyo, Wananchi wanataka waone barabara inaanza kujengwa", amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Aidha, Amekagua na Kujionea Ujenzi wa Daraja la Dharura lililopo Kata ya Sange Kijiji cha Sange.
Eng.Kasekenya amesema Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali na fedha za ujenzi wa barabara hiyo hivyo hakuna sababu yoyote ya kutokufanya kazi Kwa kasi.
Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku mbili kukagua ujenzi wa miundombinu mkoani Songwe.