Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KARAKANA YA VICHWA VYA TRENI TRC YATAKIWA KUWEKEZA KATIKA KUZALISHA WATAALAM NA VIFAA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu Mhe Seleman Kakoso ameitaka TRC Kuwekeza kwenye Karakana ili iweze kuzalisha wataalamu na vifaa ambavyo kwa sasa vinaletwa kutoka nchi za nje kwa ajili ya ujenzi,ukarabati na utekelezaji wa miradi ya Reli Nchini

Ameyasema hayo leo wakati kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea na kukagua karakana ya ukarabati wa vichwa vya Treni ya kawaida-MGR iliyopo Mkoani Morogoro

“Wekeni bajeti nzuri ambayo itasaidia karakana kutengeneza vifaa ambavyo vinawezekana kutengenezwa hapa Nchini, ukizingatia tunaelekea kipindi cha bajeti kuu ya Serikali  hivyo shirikianeni na Wizara na sisi kama kamati tupo tayari kuwaunga mkono” amesisitiza Mhe Kakoso

Kwa upande wake  Naibu Waziri Sekta ya Uchukuzi, Mhe Atupele Mwakibete amesema Serikali ya Awamu ya sita inaeendelea kutenga Fedha kwa ajili ya kukarabati vichwa na mabehewa ya treni ili kuboresha huduma ya Reli ya kati Nchini ambapo tarehe 30 juni, 2021 Serikali ya awamu ya sita iliiingia mkataba wa Dola za Kimarekani  Mil 10.5  na kampuni ya SMH RAIL kutokea nchini Malaysia kwa kutumia karakana ya Morogoro kufanya ukarabati mkubwa wa vichwa vya treni ya kawaida-MGR

‘‘Ukarabati huu ni wa kufufua vichwa vya treni ya kawaida  tisa vya Reli ya kati ambapo viwili ni vya njia kuu na saba ni vya sogeza na unaohusisha ufungaji wa vipuri vipya, Engine Mpya, Bogi mpya  na unatarajiwa kukamilika ifikapo julai,2023.” amesisitiza Mhe Mwakibete

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la reli Tanzania bi Amina Lumuli amesema Karakana ya Vichwa vya Treni Morogoro inakumbana na changamoto mbalimbali kama vile  ugumu wa upatikanaji vipuri kwa wakati,  pamoja na upungufu wa rasilimali fedha.

 Shirika la Reli Tanzania lina jumla ya vichwa vya Treni ya kawaida-MGR 59,vichwa 43 vikiwa vya njia kuu na 16 vikiwa vya Sogeza na kati yake vichwa vinavyofanya kazi ni 44 ambapo vichwa 30 ni njia kuu na vichwa 14 sogeza na limeendelea kukuza wataalamu wa ndani kwa kuwapatia ujuzi wa kimasomo ndani na nje ya nchi ili kuendana na teknolojia ya kisasa na mabadiliko ya mara kwa mara ya vipuri kwa minajili ya kuboresha usafiri wa reli ya kawaida Nchini kwa maslahi ya Taifa.