Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPA TANO TMA


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso ameiipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzanai (TMA) kwa maboresho yaliyofanywa na kuufanya utabiri unaotolewa kuaminika.

 

Akizungumza mara baada ya semina maalum kwa kamati hiyo iliyofanyika jijini Mwanza Mwenyekiti Kakoso amesema usahihi wa utabiri ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaondelea kufanywa na Serikali kwa mamlaka hiyo na kuitaka Serikali kuendelea kuwekeza ili mamlaka iendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojita kwenye utabiri.

 

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya sababu matokeo tunayaona kwa utabiri sahihi lakini pia utoaji wa taarifa umeongezeka na kuwa wa mara kwa mara, hii ni hatua kubwa sana’ amesisitiza Mwenyekiti Kakoso.

 

Mwenyekiti Kakoso ameiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), kuendelea kuwekeza zaidi kwenye vitendea na maslahi ya watumishi ili kuwapa motisha.

 

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amemuhakikishia Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye Mamlaka hiyo kwani utabiri na shughuli zote zinazofanywa na mamlaka zinaratibiwa kimataifa na ukaguzi hufanywa ili kujiridhisha na huduma zinazotolewa.

 

“Serikali imeshafunga rada 3 na rada 4 zilizobaki  zimekwisha lipiwa zaidi za asilimia 80 na zitakapokamilika na kuwasili nchini zitainua sana kiwango cha utabiri, hivyo tumejipanga vizuri kwenye kuhakikisha mamlaka inaboreshwa kwenye miundombinu", amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Agnes Kijazi ameishukuru Serikali na kusema kuwa rada 4 zilizolipiwa zitaanza kuwasili nchini kuanzia mwezi wa 7 mwaka huu.

 

Mkurugenzi Mkuu Dkt. Kijazi ameongeza kuwa kwa sasa usahihi wa utabiri baada ya maboresho kwenye miundombinu umepanda na kufikia zaidi ya asilimia 90.