Habari
KADOGOSA: TAASISI ZA DINI NI WASHIRIKA MUHIMU KATIKA MAENDELEO YA TAIFA
📌 Asema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za taasisi za dini zinazochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Mhe. Kadogosa ameyasema hayo leo, Oktoba 25, 2026, aliposhiriki na kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, mkoani Geita.
Akizungumza katika harambee hiyo ambayo Waziri Kadogosa amemwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kupitia ujenzi wa shule, zahanati na visima vya maji, pamoja na kutoa misaada kwa wananchi wanaokumbwa na majanga mbalimbali.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini ni muhimu katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Aidha, Mhe. Kadogosa amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha nchini, akieleza kuwa Wizara ya Ujenzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Amefafanua kuwa hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha barabara zinaendelea kupitika, kuzibua mifereji na mitaro ya maji, kukagua madaraja na kuandaa vifaa vya dharura ili kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa pale changamoto zitakapojitokeza.
Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Oscar Lema, amesema ujenzi wa kanisa hilo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 2.3 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Harambee hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyabiashara na waumini kutoka maeneo tofauti. Jumla ya shilingi milioni 900 zimekusanywa kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
