Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ANDAENI WAKANDARASI WA AKIBA KUELEKEA EL-NINO: KASEKENYA


Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),nchini kote kujianda  kukabiliana na athari za mvua ya elnino ili barabara zipitike wakati wote.

Ameyasema hayo Makanya Wilayani Same alipokagua maeneo korofi katika wilaya za Moshi, Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro.

"Meneja Kilimanjaro hongera kwa kazi nzuri ya kubaini na kujenga kwa ubora maeneo korofi wakati wa mvua, hakikisheni mnakuwa na vifaa na wakandarasi wa akiba ili kuwatumia haraka wakati wa dharura", amesisitiza Eng. Kasekenya.

Amesema Serikali imetoa fedha ili maeneo korofi katika barabara na madaraja nchini kote yaimarishwe hivyo kuwataka mameneja TANROADS  kusimamia vizuri ili maboresho hayo.

Amewaasa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua na kutotupa taka ovyo katika mifereji hali inayosababisha kuziba na kusababisha maji kupoteza mwelekeo na kusababisha athari kwa barabara na madaraja.

Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni ameipongeza TANROADS mkoa wa Kilimanjaro kwa uboreshaji wa barabara na madaraja katika maeneo korofi na kuahidi kuongeza elimu kwa wananchi kuelekea Elnino.

Kaimu Meneja TANROADS Kilimanjaro Eng. Benitho Mdzovela amesema wamejipanga kuhakikisha ujenzi wa maeneo korofi mkoani humo unakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

Naibu Waziri Kasekenya yuko mkoani Kilimanjaro kukagua utayari wa TANROADS kuelekea mvua za elnino ambapo pia amekagua vifaa vya dharura vitakavyotumika pindi barabara na madaraja yakiathirika wakati wa mvua.