Habari
KADOGOSA ATOA ONYO KWA MKANDARASI WA BARABARA YA KAHAMA–BULYANHULU JCT–KAKOLA
📌Asisitiza Serikali haitatoa muda wa nyongeza, ataka mradi ukamilike Desemba 2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Kahama–Bulyanhulu JCT–Kakola yenye urefu wa kilomita 73, kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ifikapo Desemba 2026, kama ilivyoainishwa katika mkataba wa mradi huo.
Kadogosa ametoa agizo hilo akiwa Msalala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakati akikagua maendeleo ya mradi huo ambao umefikia asilimia 90.17 ya utekelezaji, huku ukiwa nyuma ya ratiba iliyopangwa.
Amesisitiza kuwa Serikali haitatoa muda wa nyongeza kwa mkandarasi huyo, akieleza kuwa kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati kutasababisha hatua za kimkataba kuchukuliwa dhidi yake, ikiwemo uwezekano wa kutoshiriki katika zabuni za miradi mingine nchini kwa mujibu wa taratibu husika.
“Sitaki kuona uzembe katika barabara hii. Nataka mnihakikishie kuwa mkataba huu utakamilika kwa muda uliopangwa. Sitaongeza muda, na mkishindwa kumaliza kwa wakati, hamtapata zabuni za miradi mingine nchini,” amesema Kadogosa.
Aidha, Waziri Kadogosa amemtaka mkandarasi huyo kuongeza mitambo, vifaa na muda wa kazi ili kuharakisha utekelezaji wa shughuli zilizobaki na kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati, kwa manufaa ya wananchi na watumiaji wengine wa barabara hiyo.
Sambamba na hilo, Kadogosa amempa mkandarasi huyo siku 30 kurejesha mitambo yote iliyopelekwa jijini Arusha kutoka katika mradi anaoutekeleza mkoani Njombe. Amesema atafanya ukaguzi wa vifaa hivyo ili kujiridhisha kuwa vimerejeshwa na vinatumika ipasavyo katika utekelezaji wa mradi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kadogosa amewataka wananchi wa Msalala waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara kuondoa majengo yao kwa hiari, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokiuka taratibu za hifadhi za barabara.
Kwa upande wao, Mbunge wa Msalala, Mhe. Mabula Magangila, na Mbunge wa Kahama Mjini, Mhe. Benjamin Ngayiwa, wamesema wananchi wanatarajia kuona barabara hiyo inakamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake katika kurahisisha usafiri na usafirishaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya mkoa wa Shinyanga.
Naye, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CECC) na umefikia asilimia 90.17 ya utekelezaji.
Ameeleza kuwa mradi huo uko nyuma kwa asilimia 6.85 ikilinganishwa na asilimia 97.02 iliyokuwa imepangwa kufikiwa hadi wakati wa ukaguzi, hali inayosisitiza umuhimu wa mkandarasi kuongeza kasi ya kazi ili kukamilisha mradi ndani ya muda wa mkataba.
