Habari
FANYENI KAZI KWA UADILIFU KUONGEZA TABASAMU KWA WANANCHI: ULEGA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa maelekezo manne kwa watumishi wa Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake kubadilika na kufanya kazi kwa kasi itakayoleta matokeo chanya ili kuweza kuleta tabasamu kwa wananchi.
Akizungumza leo Novemba 20, 2025 jijini Dodoma katika kikao cha Waziri huyo na watumishi wa Wizara hiyo, Ulega amesema kuwa hatasita wala kuona huruma kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji, wasimamizi na watumishi wazembe, wavivu, wabadhilifu, wala rushwa, wenye dharau na wasiosikiliza maoni na malalamiko mbalimbali wanayopelekewa mezani.
Aidha, Ulega amewataka watumishi wa mizani kote nchini kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati ikiwemo kusikiliza malalamiko ya wasafirishaji kwa haraka na kuyafanyia kazi mapema kabla ya taarifa kufika ofisini kwake.
Ulega ameelekeza wasimamizi wanaohusika na huduma za vivuko nchini kuhakikisha wanapokea, kusikiliza na kushughulikia malalamiko yote kwa wakati na kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na zenye kuridhisha.
Ameagiza watendaji wa Wizara kusimamia haki na kutoa kipaumbele za fursa za kazi katika miradi ya ujenzi kwa makundi ya vijana na wanawake ili kunufaika na utekelezaji wa miradi hiyo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amewataka watendaji wa wizara kuhakikisha wanafanya maamuzi ya haraka katika usimamizi na utekekezaji wa miradi ya ujenzi nchini ili kuhakikisha miradi hiyo inakamikika kama ilivyopangwa.
Ametoa rai kwa watumishi hao kufanyakazi kwa ushrikiano, weledi na kwa kutambua mchango wa kila mmoja ili kufikia malengo yaliyowekwa na kutimiza azma ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde ameeleza kuwa hivi sasa Wizara inaendelea na utekelezaji wa masuala mbalimbali ikiwemo mapitio ya Sera ya Ujenzi ya mwaka 2003, mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa Taasisi zake, ujenzi wa majengo bora na nyumba za kisasa, ujenzi wa vivuko vipya Sita, matengenezo ya magari na usimamizi wa ujenzi wa madaraja ya dharura (CERC).
