Habari
DKT. MWIGULU AAGIZA SULUHU YA KUDUMU DARAJA LA MAGOLE –DUMILA
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ukaguzi wa Daraja la Magole lililopo Dumila katika Mto Mkundi wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro na kuagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto ya kujaa maji na mchanga inayolikabili daraja hilo kila mwaka.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Mei 8, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi waliofika katika eneo la daraja hilo kumsikiliza.
Amesema ni muhimu kwa TANROADS kushirikiana na wataalamu mbalimbali kuandaa mpango maalum wa kudhibiti tatizo hilo ili kulinda miundombinu ya daraja na kuhakikisha usafiri unaendelea bila usumbufu.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro kushirikiana na wataalamu wa sekta husika kuweka utaratibu utakaowaruhusu wananchi kuchimba mchanga katika eneo hilo kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu, hatua ambayo itasaidia kupunguza gharama za Serikali za uondoaji wa mchanga pamoja na kulinda daraja hilo dhidi ya athari zinazojirudia kila mwaka.
“Meneja wa TANROADS na wenzako wote ratibuni eneo ambalo tunahangaika kutoa mchanga na hatuna bajeti. Wananchi muwaruhusu watoe mchanga huo kwa utaratibu wa kitaalamu,” amesema Dkt. Mwigulu.
Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza athari za mafuriko na mkusanyiko wa mchanga katika Daraja la Magole, ambalo ni kiungo muhimu cha usafiri na uchumi kwa wananchi wa eneo hilo na mikoa jirani.
