Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

DKT. MSONDE ASISITIZA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WATUMISHI WA WIZARA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde ameisisitiza Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ya Wizara hiyo kuhakikisha inaandaa utoaji wa mafunzo kwa njia ya vitendo kwa watumisi wa Wizara hiyo ili kuleta tija kwa Wizara na Serikali kwa ujumla.

Dkt. Msonde amesema hayo leo, Februari 27, 2026 wakati akifunga mafunzo ya uandishi wa Taarifa (Report Writing) kwa Watumishi wa Wizara hiyo katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, wilayani Kibaha mkoani Pwani.

“Hakikisheni mafunzo kwa njia ya vitendo yanafanyika mara kwa mara kwani ndio yanayoleta athari chanya kwa walengwa.”, amesema Dkt. Msonde

Dkt. Msonde ameelekeza mafunzo hayo kuwa endelevu ili  kuwezesha watumishi wengine wa Wizara hiyo kujengewa uwezo, kupata uelewa na umahiri kuhusu uandaaji wa taarifa mbalimbali za Serikali.

Aidha, amewataka watumishi hao kutumia mafunzo hayo kama sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika Wizara hiyo hususan katika eneo la uandishi wa taarifa linalozingatia utaalamu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Bw. Karim Mkorehe amesema kuwa dhamira ya uongozi wa Wizara hiyo ni kuona kuwa watumishi wanapatiwa mafunzo mara kwa mara ambapo ameeleza kuwa Idara hiyo itahakikisha inaendelea kutoa mafunzo kwa kadri itakavyoweza.

Mafunzo hayo ya Siku tatu ambayo yalianza Februari 25, 2026 yameshirikisha Menejimenti ya Wizara hiyo pamoja na Maafisa mbalimbali wa Idara na Vitengo yakilenga kuwajengea uwezo watumishi hao kuhusu namna bora ya uandaaji wa taarifa mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya utumishi wa umma.