Habari
DKT. MPANGO AKAGUA UKARABATI NA UPANUZI WA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amekagua na kupokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma unaoendelea kutekelezwa Mkoani Kigoma.
Dkt. Mpango amekagua uwanja huo, leo Julai 09, 2024 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo kazi ya ukarabati na upanuzi inahusisha Ujenzi wa jengo la Abiria, maegesho ya ndege, njia za ndege, mnara wa kuongozea ndege, taa za kuongozea ndege wakati wa usiku na barabara za kuingia na kutoka uwanja wa ndege.
Dkt. Mpango ameridhishwa na kazi inayoendelea ya uboreshwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ambapo amesisitiza umuhimu wa uboreshaji wa Kiwanja hicho kwa maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
“Kigoma tunataka tufanane na wengine, tuwe na Kiwanja kizuri hata wageni wakifika Kigoma sio kale kajengo kalikoandikwa Kigoma Airport, Naamini hapa kitatoka kitu kizuri kwa hii dalili ninayoiona”, amesema Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango amewataka wananchi waliopata fursa za ajira katika mradi wa ujenzi na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa kwa manufaa ya Mkoa na Taifa.
“Wananchi wa Mkoa huu ni waaminifu sana kwa hiyo ninyi endeleeni kuchapa kazi na Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwa miradi inayokuja lazima iwanufaishe wananchi”, amesisitiza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemueleza Makamu wa Rais kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), imejipanga kufidia muda uliochelewa katika utekelezaji wa uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma na kukimalisha ifikapo mwezi Disemba, 2025.
Bashungwa ametaja changamoto zilizoukabili ucheleweshaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ikiwemo ya Mvua, uzembe wa Mhandisi Mshauri na Wizara ikachukua jukumu la kumbadilisha na sasa hivi kazi za ujenzi zinaendelea kwa kasi ili kufidia muda uliopotezwa.
“Kwa mujibu wa mkataba tulitakiwa tukabidhi uwanja huu mwakani mwezi wa tatu lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza tunahidi mwakani mwezi Disemba tutakuwa tumekamilisha jengo la abiria, pamoja na maegesho ya ndege” amesema Bashungwa.
Aidha, kuhusu upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja hicho Bashungwa ameeleza kuwa sasa hivi barabara hiyo ina urefu wa mita 1,800 na Wizara ya Uchukuzi inaendelea na utaratibu wa kuiongezea urefu hadi kufika mita 3,100 ili kuwezesha ndege aina yoyote kutua bila changamoto yoyote.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa ukarabati na uboreshaji wa kuinua hadhi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma utahusisha ujenzi wa jengo la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuchukua abiria 69,000 hadi 129,000 kwa mwaka.
Ameongeza kuwa mradi wa uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma unatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya China Railway Engineering Group na Mhandisi Mshauri kampuni ya M/s Khatib & Alami Consulting Engineers - off shore S. A. L ya Lebanon ikishirikiana na kampuni ya Advanced Engineering Solutions ya Tanzania.