Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

CHANGAMKIENI FURSA ZA UWEKEZAJI UKANDA WA BAHARI YA HINDI: KASEKENYA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya ametoa rai kwa watanzania kuwekeza kikamilifu katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara hususan ukanda wa bahari ya Hindi katika mikoa ya Tanga na Pwani.

Rai hiyo ameitoa Septemba 18, 2024 alipokagua ujenzi wa barabara ya Tanga- Pangani-Saadani-Bagamoyo hadi Dar es salam (sehemu ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange (Km 95.2) na kusisitiza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua uchumi wa Tanzania kutokana na vivutio vilivyopo katika ukanda huo hivyo ni vyema wananchi wakachangamkia fursa mapema wakati ujenzi ukiendelea.

"Barabara hii ya Dar es Salaam-Bagamoyo-Pangani-Tanga ni sehemu ya barabara ya Africa Mashariki inayoanzia Malindi- Lungalunga-Horohoro-Bagamoyo hadi Dar es Salaam, ikikamilika itachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania hususan utalii, uvuvi, biashara na huduma za uchukuzi hivyo ni wakati wa kila mtanzania kuangalia fursa katika ukanda huu", amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amemtaka Mkandarasi China Railway 15 B. Group anayejenga sehemu ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange (Km 95.2) kuhakikisha sehemu hiyo inakamilika ifikapo Machi mwakani na kusisitiza Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Tanga kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi kuongeza vifaa, wataalam na muda wa kazi ili kukidhi mahitaji ya mkataba.

Amefafanua kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho kuanza kujenga barabara ya Kwamsisi-Mkata KM 38, ambayo ni muendelezo wa barabara hiyo Wilayani Handeni, Kange na Makurunge kwa upande wa Wilaya ya Bagamoyo hivyo kuwataka wananchi katika maeneo ya mradi huo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi pindi kazi itakapoanza.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na barabara unganishi (Km 14.3) na kumtaka Mkandarasi Shandong Luqiao Group kufanyakazi usiku na mchana ili kufikia lengo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi huo Samson Ejigu amesema barabara hiyo itakapokamilika itakuwa na madaraja makubwa manne, makalvati makubwa 30 na madogo 148 yatakayowezesha maji kupita kwa urahisi na hivyo kutoathiri barabara hiyo.