Habari
BILIONI 2.5 ZILITUMIKA KULIPA FIDIA KWA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA BARABARA YA KIDATU – IFAKARA

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ililipa fidia jumla ya Shilingi 2,576,081,789.00 kwa wananchi 142 waliopisha ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 67) ,kwa Wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5.
Hayo yameelezwa leo Septemba 3,2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilombero Abubakar Asenga aliyeuliza Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa barabara ya Kidatu kwenda Ifakara km 67.
"Zoezi la Ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 67) lilifanyika mwaka 2017 kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007", amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa kwa wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara hawakustahili fidia kwa mujibu wa sheria.
Aidha, kuhusu Upanuzi wa barabara ya Mombo - Lushoto, Waziri Bashungwa amesema Serikali imekamilisha kazi ya Upembuzi uakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami na upanuzi wa barabara ya Mombo hadi Lushoto yenye urefu wa kilometa 31.36 ambapo kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hiyo.
Waziri Bashungwa amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Lushoto Shabani Shekilindi aliyeuliza Je, lini Serikali itafanya upanuzi wa barabara ya Mombo hadi Lushoto kwa kuwa ni nyembamba sana kiasi cha magari makubwa kushindwa kupita.