Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA: BARABARA APP SULUHU LA MIUNDOMBINU YA BARABARA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara nchini kupitia mfumo wa kieletroniki wa ‘Barabara App’ ili hatua za haraka kwa barabara zinazohitaji matengenezo ziweze kuchukuliwa.

Amesema kupitia mfumo huo, watumiaji wa barabara wanaweza kushiriki katika kusimamia miundombinu ya barabara katika maeneo wanayoishi au kupita kwa kutuma taarifa muhimu za hali ya barabara katika Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), ambapo Bodi hiyo itawasilisha mahala husika katika Taasisi ya Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Ametaja miongoni mwa taarifa hizo ikiwemo barabara kujifunga, daraja au kalvati kubomoka/ kuzolewa na mafuriko, mashimo hatarishi barabarani, kazi kufanyika chini ya kiwango, mitaro kuziba na hujuma zozote zinazofanyika katika miundombinu ya barabara.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma wakati akihitimisha ziara yake katika Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) ambapo Waziri huyo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo.

“Niwaombe watanzania kutumia mfumo huu unaomwezesha mwananchi kutoa taarifa ya hali ya miundombinu ya barabara yenye changamoto, au hujuma yoyote maeneo anayoishi”, amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameongeza kuwa lengo la kuwa na mfumo huo ni kuipunguzia Serikali gharama kubwa za matengenezo ambayo ingeia kutokana na uchelewaji wa matengenezo hayo.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vyema kuhakikisha Taasisi ya Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) inayosimamia barabara kuu na za mikoa na ile ya Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), inayosimamia barabara za Halmashauri/ Wilaya wanajipambanua zaidi katika kuhudumia barabara zote nchini.

Amewataka watanzania kuwa na imani na taasisi hizo katika kuhudumia na kusimamia mtandao a barabara nchini kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu yao.

“Ningependa kuwajulisha watanzania kuwa huko nyuma kulikuwa na maombi makubwa ya barabara ambazo zipo kwenye wilaya zetu ili zipandishwe hadhi kuja TANROADS, lakini hivi sasa hilo hitaji ni kama limeisha kwasababu TARURA imekwisha jengewa uwezo na kuimarishwa mfuko wake”, amefafanua Bashungwa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo, Kaimu Mtendaji wa RFB Eng. Rashid Kalimbaga, ameeleza kuwa mbali na mfumo wa kieletroniki wa kufuatilia barabara Bodi imeimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuzuia matumizi mabaya ya fedha.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutaziba mianya ya uvujaji wa mapato pamoja na uchakachuaji katika ujenzi na matengenezo ya barabara.