Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AKAGUA UJENZI BARABARA YA LAMI YA BUGENE – BENACO


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inamlipa kwa wakati Mkandarasi M/s China Road and Bridge Cooperation anayejenga barabara ya Bugene – Kasulo (Beneco) – Kamunazi (km 128.5) kwa kiwango cha lami sehemu ya Bugene – Burigi Chato yenye urefu wa kilometa 60.

Amesema hayo Oktoba 12, 2023 wakati  akizungumza na wananchi wa kata ya Nyaishozi mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kulipa kwa wakati madai mengine yatakayowasilishwa na mkandarasi huyo ili aweze kuongeza kasi ya ujenzi pamoja na kulipa fidia kiasi cha bilioni 2 kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo.

“Kuhusu fidia naomba niwaambie, mtupe kama mwezi mmoja kuanzia hii leo,  tutakuwa tumekamilisha na hizo bilioni 2.074 zitakuwa zimeshakuja ndani ya wilaya ya Karagwe na wale ambao mmesubiri kwa muda mrefu tunaenda kuweka historia” amesema Bashungwa.

Bashungwa amewataka wananchi wa kata ya Nyaishozi kujipanga na kuhakikisha wanaweka mipango miji vizuri kwani Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaleta maendeleo kupitia miundombinu ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwenda nchi za jirani.

Aidha, Bashungwa wakati  akikagua eneo la mlima kihanga, kuangalia changamato zinazowapata watumiaji wa vyombo vya moto katika mlima huo na kuahidi kuwa wizara itafanya haraka kutatua changamoto katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa Madereva wanaoendesha vyombo vya moto kuheshimu tahadhari na onyo ambazo zinatolewa kwenye vibao ambavyo vimewekwa barabarani kwani vimewekwa ili kulinda na kusaidia usalama barabarani.

"Umahiri wa dereva sio kukimbia sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine, bali ni kuhakikisha abiria  waliopo kwenye chomba chake wapo salama, hivyo pamoja na marekebisho ambayo sio suluhisho kwa asilimia 100 bado  madereva wanatakiwa kuhakikisha wanazingatia masuala ya usalama barabarani ikiwemo kuacha tabia ya mwendo kasi ", ameongeza Bashungwa.

Awali akitoa taarifa ya kukabiliana na tatizo la ajali eneo mlima Kihanga, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Kagera Eng. Ntuli Mwaikokesya amesema kuwa wamejipanga  kuongeza alama za tahadhari pamoja na kuweka taa sita kwenye eneo hilo ili alama hizo ziweze kuonekana nyakati za usiku hususani kwa madereva wageni ambao hupata ajali mara kwa mara.

Kuhusu barabara ya Bugene - Burigi Chato Eng. Mwaikokesya amesema kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 27.7 na kwamba mara baada ya malipo hayo kufanyika Mkandarasi ataongeza timu za ujenzi wa barabara na makalvati pamoja na kufanya kazi usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea.

Ukaguzi wa miradi inayoendelea ni muendelezo wa ziara ya Waziri Bashungwa  kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara yake katika mikoa mbalimbali nchini aliyoanzia mkoani Mbeya, Iringa, Singida, Simiyu, Mara, Mwanza na Kagera kuona maendeleo ya miradi hiyo na  hatua za utekelezaji wake sambamba na ubora wa kazi zinazoendelea katika miradi hiyo.