Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AKAGUA ATHARI ZA MVUA KILIMANJARO, ATOA MAELEKEZO KWA MAMENEJA WA TANROADS.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua athari za mvua za El-Nino katika mji wa Hedaru na Saweni wilayani Same na kutoa pole kwa Wananchi ambao wameathirika na mvua zilizonyesha usiku na kusababisha maji na tope kujaa kwenye nyumba zao, nyumba za ibada na miundombinu ya barabara.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, leo tarehe 24 Novemba 2023, Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa Kilimanjaro kuhakikisha magogo, takataka na tope vilivyosambaa katika nyumba hizo na barabara kuu ya Tanga kuelekea Kilimanjaro viondolewe haraka ili Barabara ipitike wakati wote.

Bashungwa amezungumzia umuhimu wa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati mvua zinaendelea kunyesha no katika maeneo hayo na kumtaka Meneja wa TANROADS kuongeza idadi ya wakandarasi ili kazi ya kusafisha mitaro pamoja na kufuatilia mikondo ya maji milimani ili kudhibiti takataka, maji na magogo yasishuke kwa kasi katika makazi ya watu na barabarani.

Aidha, Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANROADS, kuwawezesha mameneja wa mikoa ili kukabiliana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha ili zisiharibu miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote.

Amewataka Mameneja na wataalamu wao kufanya ukaguzi wa maeneo ya madaraja na barabara kila wakati ili kubaini na kudhibiti mapema athari zinazoweza kujitokeza kufuatia mvua hizo.

"Hakikisheni mnashirikiana kwa karibu sana na Mamlaka za Serikali za Mikoa, Wilaya  na mitaa ili kupata taarifa sahihi za madaraja na barabara na kuzipatia ufumbuzi  kwa wakati", amesisitiza Waziri Bashungwa.

Amewataka  Mameneja wa TANROADS Mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha kukaa pamoja na kufanya tathimini katika maeneo yaliyoathirika na yanayoweza kuathirika ili huduma ya usafiri iwepo wakati wote.

Bashungwa amekemea tabia za baadhi ya wananchi kutoa taarifa zisizo sahihi zinazoweza kusababisha taharuki kwa wasafirishaji na wasafiri.
Amewapongeza Mameneja wa TANROADS wa  Mikoa ya Tanga, Pwani na Kilimanjaro kwa kuchukua hatua za haraka katika maeneo yaliyoathirika na kuwataka mameneja wote nchini kuhakikisha barabara na madaraja yanakuwa salama wakati wote.

"TANROADS makao makuu hakikisheni mnawalipa kwa haraka makandarasi wanaofanya kazi za dharura na kuepuka wakandarasi wanaoongeza bei wakati kazi zinaendelea na wale ambao barabara wanazojenga zinaharibika kwa muda mfupi”, amesisitiza Bashungwa.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohammed Besta ameitaja Mikoa ya Dar  es salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Songwe kuwa miongoni mwa mikoa iliyoathirika zaidi na athari za mvua za El - Nino lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote.
Waziri Bashungwa anaendelea na ziara yake ya kukagua miundombinu  na athari mvua za El-Nino mkoani Kilimanjaro.