Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA KIDATU-IFAKARA KUKAMILIKA MEI


Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi  Reynolds Construction Company Nigeria ltd, anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa KM 66.9 pamoja na daraja la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mwezi Mei mwakani.

Amesema changamoto zote zilizokuwa zikichelewesha mradi huo zimepatiwa ufumbuzi hivyo kazi iliyobaki ni kwa Mkandarasi kukamilisha ujenzi.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Eng. Kasekenya amesema barabara hiyo itakuza kilimo katika mkoa wa Morogoro na ukanda wa kusini mwa Tanzania, kupunguza muda wa usafiri na gharama za kusafirisha mazao na pembejeo za kilimo, kuongeza thamani ya mazao na hivyo kukuza uchumi wa wananchi kwa ujumla.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaufungua mkoa wa Morogoro ambao ni ghala la chakula ili kuunganisha kwa njia fupi na mikoa ya Njombe na Ruvuma,” amesema Naibu Waziri huyo.

Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Kitengo cha Uhandisi Ushauri cha TANROADS (TECU), kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji kuboreshwa ili kuimarisha usalama katika barabara hiyo yanafanyiwa kazi haraka na kwa viwango.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Lazack Kyamba amesema mradi huo ambao umefikia asilimia 68 uko katika hatua nzuri na watamsimamia mkandarasi ili ukamilike kama ilivyopangwa.

Barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ni sehemu ya barabara ya Mikumi-Ifakara yenye urefu wa KM 130 inayopita katika ukanda wenye uzalishaji mkubwa wa mazao hivyo kukamilika kwake kutaboresha ustawi wa jamii kwa kukuza uchumi wa watu na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Dumila –Kilosa- Mikumi KM 142, sehemu ya Rudewa-Kilosa KM 24 ambayo inajengwa na wakandarasi wazawa na kuwataka waongeze bidii ili kujenga imani kwa Serikali.

Kampuni hiyo ya Umoja-Kilosa JV inajumuisha kampuni saba za kihandisi za wazawa ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili kumudu kujenga miradi mikubwa na hivyo kunufaika kiuchumi na kiuzoefu.

“Barabara hii ya Dumila-Kilosa-Mikumi inayopita nje ya mbuga ya wanyama ya mikumi itakapokamilika itapunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro-Iringa na kupunguza ajali za magari kugonga wanyama katika mbuga hiyo,” amesema Eng. Kasekenya.

Msimamizi wa mradi huo Eng. Protas Mwasyoke amesema wamejipanga kuhakikisha sehemu iliyobaki ya kuunganisha kwa lami barabara ya Dumila-Rudewa –Kilosa inakamilika ifikapo Machi mwakani.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Morogoro kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za lami.