Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BADO KM 51.1 KUUNGANISHA TABORA-KIGOMA KWA LAMI


IMEELEZWA kuwa bado kilomita 51.1 ili kuunganisha mikoa ya Tabora na Kigoma kwa barabara ya lami na hivyo kuandika historia ya aina yake nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tabora- Kigoma sehemu ya Kazilambwa-Chagu yenye urefu wa KM 36 na Malagarasi-Ilunde-Uvinza KM 51.1.

“Kwa kweli nimeridhika na kasi ya ujenzi sehemu ya Kazilambwa-Chagu yenye urefu wa KM 36 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 99”, amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemtaka mkandarasi STECOL Cooperation Ltd anayejenga sehemu ya Malagarasi-Ilunde-Uvinza KM 51.1 kufanya kazi usiku na mchana ili kuandika historia ya kuunganisha mikoa ya Tabora na Kigoma kwa lami mapema iwezekanavyo.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amesema ujenzi huo umefikia asilimia 45 na watamsimamia kikamilifu mkandarasi ili maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua yakamilishwe mapema ili kuepuka visingizio na  kuwawezesha wasafiri na wasafirishaji wa mikoa hiyo kunufaika na barabara ya kisasa.

Zaidi ya shilingi bilioni 62.7 zinatumika katika ujenzi huo ambazo ni matapo ya ndani na mkopo nafuu kutoka mifuko ya OPEC na Abu Dhabi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amemtaka Mbunge wa Urambo Mhe. Margareth Sitta kuhamasisha wananchi wa jimbo hilo kulinda miundombinu inayojengwa katika jimbo hilo ikiwemo taa na alama za barabarani ili kuepusha ajali na kuendana na kasi ya Serikali ya kupendezesha barabara nchini.

“Tunawajengea barabara na mzunguko wa kisasa round about ili kupunguza ajali eneo lililokuwa na kona kali na kutengeneza taswira nzuri ya Urambo hivyo hakikisheni miundombinu hii inalindwa na kuendelezwa kwani inatumia fedha nyingi za Serikali “, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Kwa upande wake Mhe. Margareth Sitta ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kisasa katika wilaya ya Urambo na kuahidi kutoa elimu kwa wananchi kuthamini uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Awali Naibu Waziri Kasekenya amemtaka Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group (BECG), anayejenga jengo la abiria na mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Tabora kuongeza kasi ya ujenzi kwani Serikali imedhamiria kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania kwa miundombinu yote ya ardhini, majini na angani ili kuwawezesha wawekezaji na wazalishaji kuibua fursa zilizoko katika ukanda huo na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.