Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ATCL WATAKIWA KUANGALIA UPYA NAULI


Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete ameitaka Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutazama upya gharama za tiketi kwa safari za ndani ya nchi ili kuvutia wasafiri wengi kutumia usafiri wa shirika hilo.

 

Akizungumza mkoani Katavi baada ya kutembele Kiwanja cha Ndege cha Mpanda Naibu Waziri Mwakibete amesemaa uwepo wa gharama kubwa za tiketi unachangia uchache wa abiria wanaotumia shirika hilo pamoja na  takwimu kuonyesha ongezeko la abiria kwa safari za ndani kupitia kiwanja hicho.

 

“Takwimu nilizosomewa hapa zinaonyesha ongezeko la abiria kwa safari za ndege lakini naambiwa hapa abiria bado wapo wa kutosha lakini wanakwazwa na na gharama za nauli, mkiangalia upya nina Imani mnaweza kuleta ndege karibu kila siku ‘ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

 

Naibu  Waziri Mwakibete amesema Serikali imeichukua changamoto ya udogo wa jengo la abiria kiwanjani hapo na kuahidi kuwa itatafuta fedha ili kujenga jengo litakaloendana na hadhi ya kiwanja hicho.

 

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewataka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kujenga barabara itakayotumika kukagua eneo lote la kiwanja ili kupunguza changamoto za shughuli za kibinadamu zinazohatarisha usalama kiwanjani hapo.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusufu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita  kwa kuhakikisha ATCL inaongeza safari zake mkoani humo kutoka safari moja kwa wiki mpaka kufikia safari nne kwa wiki uamuzi uliorahisisha shughuli za kibiashara biana ya mkoa huo na mikoa mingine.

 

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege Mpanda Jeff amesema TAA inaendelea kuhakikisha kiwanja hicho kinatoa huduma stahiki kulingana na kanuni na taratibu za usafiri wa Anga Duniani.

 

Meneja wa ATCL Mkoa wa Mpanda Salehe amesema pamoja na changamoto za kiwanja kutokuwa na kituo cha mafuta ATCL itaendelea kutoa huduma huduma bora na za viwango kupitia kiwanja hicho.