Habari
WIZARA YA UJENZI YAWEKA MSISITIZO MATUMIZI YA DATA SAHIHI KUFIKIA DIRA 2050
Wizara ya Ujenzi imewataka Wakurugenzi na Mameneja wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) katika taasisi zilizo chini yake kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuongeza ufanisi, ufuatiliaji, na mgawanyo wa rasilimali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Ujenzi, Bi. Veila Shoo, wakati akifunga kikao cha robo ya kwanza cha Wakurugenzi na Mameneja wa Ufuatiliaji na Tathmini kilichofanyika jijini Dodoma.
Shoo amesema upatikanaji wa takwimu sahihi na taarifa zenye ubora ni muhimu katika kuwezesha Serikali kufanya maamuzi sahihi, kufuatilia matumizi ya fedha za umma na kupima matokeo ya miradi inayotekelezwa katika sekta ya ujenzi.
“Hatutaweza kufikia Dira 2050 kama hatuna data sahihi. Kazi yetu sisi ni kuhakikisha kila shilingi inayotumika katika ujenzi inafuatiliwa na ina matokeo yanayoonekana kwa wananchi,” amesema.
Kikao hicho kimewakutanisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, zikiwemo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB).
Taasisi zingine ni Bodi ya Usaji wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Vikosi vya Ujenzi (CSWS) na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT).
Katika kikao hicho, washiriki walijadili mada tatu kuu ambazo ni nafasi ya sekta ya ujenzi katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, usimamizi wa mipango ya kitaifa pamoja na hali ya ufuatiliaji na tathmini katika sekta hiyo.
Wakati wa majadiliano kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ilielezwa kuwa sekta ya ujenzi ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda na kuhakikisha maendeleo endelevu.
Washiriki walisisitizwa umuhimu wa kupanga na kutekeleza miradi ya kimkakati ya miundombinu, ikiwemo barabara na majengo ya kisasa kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu ya Taifa.
Katika mada ya usimamizi wa mipango ya kitaifa, kikao kilijadili umuhimu wa kuhakikisha mipango ya sekta ya ujenzi inaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa pamoja na miongozo inayotolewa na Tume ya Mipango.
Aidha, kikao kiliazimia kuanzisha mfumo wa pamoja wa taarifa utakaotumiwa na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, hatua inayotarajiwa kuboresha upatikanaji wa takwimu na kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi.
Aidha, washiriki walikubaliana kufanya mapitio ya Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji katika Sekta ya Ujenzi ili kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na upimaji wa matokeo ya miradi.
Maazimio hayo yanatarajiwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
