Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI MBARAWA AMTAKA MKANDARASI SONGORO KUMALIZA UKARABATI MV KAZI KWA HARAKA.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Profesa Makame Mbarawa amemataka mkandarasi Songoro Marine Boatyard kuhakikisha anamaliza haraka ukarabati anaoufanya kwenye kivuko cha MV. KAZI ili kiweze kurejea  kutoa huduma katika kivuko cha Magogoni Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 

Profesa Mbarawa ametoa maagizo hayo mapema leo wakati alipotembelea eneo la Yadi ya Songoro Kigamboni Jijini Dar es Salaam kukagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho ambacho kwa mujibu wa mkandarasi kinatakiwa kurejea kutoa huduma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

 

‘’Mpaka sasa tumeona kazi imefanyika, na nikushukuru sana mkandarasi kwa kufanya kazi hiyo, niwashukuru pia TEMESA kwa usimamizi mzuri, na kama ulivotuahidi  kwamba baada ya vifaa vyote kufika utafanya kazi usiku na mchana ili mwishoni mwa mwezi wa tisa kazi hii ya ukarabati kivuko cha MV. KAZI iwe imekamilika’’ Alisema Profesa Mbarawa.

 

Aidha Profesa Mbarawa  ameitaka TEMESA pia kuangalia namna ya kushirikiana na taasisi binafsi ili kuanza kutoa huduma ya pamoja katika eneo la Magogoni na Kigamboni ili kurahisisha utoaji wa huduma katika eneo hilo.

 

‘’Wakati umeshafika sasa tubadilishe mfumo wetu, sea taksi zile zilizopo pale kivukoni sasa ziwe za kudumu na wananchi waweze kuchagua kama wanataka kwenda na kivuko na wale wenye safari za haraka waweze kutumia sea taksi na ninavoona huko mbele tuweke taasisi binafsi ziweze kushirikana kutoa huduma hii’’, amesisitiza Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa anaamini taasisi binafsi wakishirikiana na TEMESA ushindani utakuwa mkubwa na huduma zitakuwa bora zaidi na kwa haraka zaidi.

 

Naye Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na KusiniMhandisi Lukombe King’ombe akizungumza wakati wa zoezi hilo amesema mkandarasi tayari ameshamaliza kubadili mabati ya chini ya kivuko hicho, kupaka rangi za mwanzo kwenye deki na maeneo mengine ya kivuko huku wakisubiri kutoa vipuri bandarini.

 

‘’Maelekezo yetu kwa mkandarasi ni atakapotoa vipuri basi afanya kazi usiku na mchana ili ikiwezekana tuikamlishe chini ya Mkataba ambayo ilikuwa ni wiki ishirini’’. Alisema Mhandisi King’ombe.

 

Aidha Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Khalid Songoro naye amesema vifaa vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi zikiwemo injini za kivuko vitafika mwisho wa mwezi huu (Agosti) pamoja na kontena ambalo tayari limefika bandarini likiwa na milango ya mbele pamoja na vifaa vingine ambavyo vililetwa na ndege kwa ajili ya kufanya ovaholi ya pampu jeti na zitaanza kufanyiwa kazi hiyo haraka iwezekanavyo.