Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WATUMISHI WAPYA MIZANI WATAKIWA KUWA WAZALENDO


Watumishi wa Mizani nchini wametakiwa kuwa  wazalendo, wachapakazi na wanaofanyakazi kwa weledi ili kulinda barabara na kuzifanya zidumu kwa muda mrefu.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Bw, Albert Msovela wakati akifungua semina ya mafunzo kwa watumishi wapya wa mizani wa Mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora mjini Mpanda.

Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yatawajengea uwezo watumishi hao wa mizani kuhusu elimu ya Sheria  ya  udhibiti uzito wa magari ya mwaka 2016 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki   na kanuni zake za mwaka 2018 

Bw, Msovela amesema Serikali inatumia fedha nyingi sana katika kutekeleza miundombinu ya barabara na madaraja kwa kutumia wataalamu katika ujenzi wake ili kuwa na miundombinu bora hivyo watumishi wanapaswa kuzingatia sheria hiyo kwa kutoa huduma bora kwa wateja ili kulinda barabara na kuepuka gharama za matengenezo ya mara kwa mara.

Katibu Tawala huyo amesema miundombinu ya mikoa yote nchini imetengenezwa kitaalamu na  kuunganishwa kwa kiwango cha lami  ambapo inarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wasafiri na wasafishaji na jamii kwa ujumla ambapo huchochea  kuleta maendeleo katika taifa

"Fanyeni kazi kwa kusimamia sheria na uzalendo  kuwa na uadilifu,uaminifu pamoja na kufuata taratibu,kanuni na miongozo kutoka kwa viongozi ili kulinda miundombinu ya barabara, "amesisitiza Msovela.

Aidha, amewasisitiza watumishi hao kutoa huduma bora kwa wateja  ili  kuepukana na rushwa na kutumia muda mwingi kujifunza  na  kuelewa Sheria hiyo na kanuni zake  kupitia wataalam katika mafunzo hayo

Ikumbukwe kuwa Mafunzo hayo yanalenga  kuwakumbusha watumishi wote wa mizani kufahamu na kuzingatia Sheria ya kuthibiti uzidishaji uzito wa magari barabarani wa Kanda ya magharibi ambapo yanafanyika kwa siku nne.