Habari
WATUMISHI WA MIZANI WAASWA KUZINGATIA SHERIA
Meneja Mizani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Leonard Mombia amezungumzia umuhimu wa watumishi wa Mizani kuzingatia na kufuata sheria ya kudhibiti uzito wa magari pamoja na kutekeleza taratibu na kanuni zilizowekwa ili kulinda na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja
Mhandisi Mombia amesema hayo leo mjini Mpanda wakati akifunga mafunzo endelevu ya sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 yaliyomalizika leo Mkoani Katavi
Amesema kwamba Serikali ya awamu ya sita inaendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi ya barabara kwa kiwango cha lami ambapo mizani zimejengwa kimkakati ili kudhibiti uzito wa magari na kuzuia uharibifu wa barabara na madaraja
"Kupitia mafunzo haya nendeni mkawe mabalozi kwa watumishi na wasafirishaji kwa kuzingatia Sheria taratibu na kanuni zilizopo na kuleta matokeo chanya katika kulinda barabara zetu "Amesema Mhandisi Mombia
Aidha ametoa Rai kwa watumishi na wasafirishaji wa Kanda ya magharibi kuepuka vitendo vya rushwa ambavyo ni kinyume cha sheria ya nchi na kuwajibika kwa kufanya kazi kwa weledi
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi Eng.Martin Mwakabende amewashukuru wataalam wa Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kuandaa maf unzo hayo muhimu na endelevu kwa watumishi ambapo yatawawezesha kusimamia vizuri sheria ya mizani na kutoa elimu ya kulinda barabara na madaraja
Mafunzo hayo ya siku nne yalianza tarehe 28/10/2024 na kumalizika 31/10/2024 Mkoani Katavi ni muendelezo wa Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuwajengea uwezo wataalam wa mizani nchini kote ili kufanya kazi kwa weledi na kuleta tija katika sekta ya usafiri na uchukuzi nchini kote.