Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Wasafirishaji nchini wahimizwa kutii sheria


Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila wakati akifungua mafunzo ya utoaji elimu kwa wasafirihaji juu ya upimaji uzito wa magari kwa kutumia Sheria ya Afrika Mashariki ya kudhibiti uzito ya mwaka 2016.

Mhandisi Mativila amewaambia waandishi wa habari kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa uelewa wa sheria ya udhibiti uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 na kwamba jukwaa hilo litatumika kupokea maoni, ushauri na namna mapendekezo namna bora ya kuendelea kuboresha utendaji kazi.

"Niwaase wasafirishaji wote kutii sheria katika utendaji wa kazi zenu lakini pia niwatake watendaji wetu kutoa huduma kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kwa umoja wetu tuendelee kutunza barabara zetu kwa kubeba uzito unaokubalika," amesema Mhandisi Mativila.

Aidha ameongeza kuwa ni imani ya serikali kwamba baada ya mafunzo hayo makosa ya uzidishaji uzito wa magari barabarani yatapungua au kuisha kabisa.

Kwa upande wake msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Saukwa amesema kuwa semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo wasafirishaji na wamiliki wa magari ya mizigo ili  waweze kuelewa sheria ya udhibiti  uzito ya Afrika Mashariki na kanuni zake na kwamba watazunguka nchi nzima katika vituo 13 kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.

Aidha mmoja kati ya wadau wa usafirishaji anayeshiriki mafunzo hayo amesema kuwa uelewa juu ya sheria hiyo utawasaidia kudhibiti uzito kwenye magari ya usafirishaji hatua itakayosaidia kulinda barabara za ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Mafunzo hayo ambayo yanashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji yamepangwa kufanyika katika Mikoa 13 ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Njombe, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Geita, Tabora, Mwanza, Arusha na Tanga.

Sheria hiyo inatumiwa na nchi zote za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

Imetolewa na, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi